January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mukya ataka TBS iongezwe watumishi

Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Joyce Mukya (kulia) akiwa na Joshua Nassari Mbunge wa Arumeru Mashariki

Spread the love

MBUNGE wa Viti Maalum, Joyce Mukya (Chadema), ameitaka Serikali kuongeza watumishi zaidi kwenye Shirika la Viwango nchini (TBS) ili kukabiliana na watu wanaoingiza bidhaa feki kupitia mipakani. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Mukya ametoa kauli hiyo leo bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza, ambapo amesema vipodozi vingi na bidhaa zingine zinaingiza nchini kupitia njia za panya.

Amesema TBS ina watumishi 230 ikilinganisha na KBS ya Kenya ambayo ina watumishi 1000 na Tanzania ina mipaka mingi sana ya kuingia vipodozi na bidhaa zingine ukilinganisha na Kenya yenye mipaka michache. 

“Serikali haioni umuhimu wa kuongeza wafanyakazi katika shirika hili? Amehoji Mukya.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe, amekiri kuwepo kwa upungufu wa watumishi nchini ikiwemo TBS.

Amesema kutokana na tatizo la upungufu wa watumishi, serikali itaendelea kuongeza watumishi ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Wizara wa Viwanda na Biashara. 

Awali, katika swali la msingi, Mbunge Mji Mkongwe, Muhammad Ibrahim Sanya (CUF), amehoji ni lini serikali itakuwa makini katika kuzuia bidhaa za vipodozi zisiendelee kuingizwa nchini. 

Akijibu swali hilo, Dk. Kebwe amesema jitihada mbalimbali zilikuwa zikichukuliwa kudhibiti uingizaji wa vipodozi nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vilivyojiliwa ndivyo vinaingia na kutumika.

Amesema hadi sasa TFDA imesajili jumla ya vipodozi 2,527 ambavyo ndivyo vinaruhusiwa kuingizwa na kutumika nchini.

error: Content is protected !!