August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Muhongo aufyata, Wananchi walia

Jiji la Dar es Salaam linavyoonekana usiku kutokana na taa zilizowashwa kwenye majumba

Spread the love

TAMBO za Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini kwamba, ‘umeme hautapanda, mimi ndio waziri nimesema’ zimefika kikomo, anaandika Josephat Isango.

Jana Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imeridhia kupanda kwa gharama za umeme. Ridhaa hiyo inakwenda sambamba na baraka za Prof. Muhongo.

Kupanda kwa umeme kulikotangazwa na Felix Ngamlagozi, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura kunazima tambo za Prof. Muhongo kwa wananchi kuwa ‘umeme hautapanda’.

Mwandishi wa habari hii amemtafuta Prof. Muhongo kutaka kujua sababu za ahadi yake ya kutopandisha umeme kutoendelea kuwa hai, hata hivyo simu yake haikupokewa.

Ngamlagozi amesema kuwa, wateja wa kundi la T1A na ambao matumizi yao ni ya kawaida, wateja wa nyumbani na taa za barabarani watauziwa kwa Sh. 312 badala ya 388 kama ilivyopendekezwa na Tanesco.

Kundi T1B wakiwa ni wenye viwanda vidogo, mabango na minara ya simu watauziwa kwa Sh. 317 kwa uniti badala ya 340 kama ilivyopendekezwa na Tanesco.

Kwa wakati tofauti Novemba mwaka huu serikali ilieleza kitendo cha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupandisha bei katika kipindi kifupi si sahihi kiuchumi.

Na kwamba, haileti tija kwa wananchi na wafanyabiashara kwani inafanya bei za umeme kutotabirika.

Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau ulioandaliwa na Ewura mjini Dodoma, Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Serikali, Ezamo Maponde alisema, baraza hilo limefanya uchambuzi wa kina uliowasilishwa na Tanesco.

Na kuwa, Tanesco iliomba kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 18.19 na kubaini kuwa, katika maombi hayo shirika hilo la umeme limeonesha maombi yao ni ya mwaka moja tu wa 2017 ambapo ni tofauti na utaratibu uliowekwa na Ewura wa kupitisha bei za miaka mitatu.

Ni katika wiki hiyo ndiyo Prof. Muhongo alisema, ili kujenga nchi ya viwanda inahitajika umeme wa uhakika wenye bei rahisi.

Aliitaka Tanesco kukaa naye wakiwa wamejifungia kujadili kuhusu masuala mengine wanayotaka shirika hilo ikiwemo gharama ya umeme.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme katika Jiji la Dar es Salaam Prof. Muhongo alisema, “tunachohitaji ni umeme wa uhakika na bei rahisi na hili la gharama ya umeme tutaongea tukijifungia mimi na Tanesco.”

Alisema kutokana na uboreshaji huo, kwa sasa hawataki mgawo wa umeme kwa kuwa Watanzania wamechoka kukatikakatika kwa umeme.

Wananchi si ‘shamba la bibi’ mkoani Arusha, wadau wamepinga bei hiyo na kuitaka Tanesco isiwageuze wananchi kama shamba la bibi kwa ajili ya shirika hilo kwa kuwaongezea bei ya nishati hiyo.

Mafutah Bunini, Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Serikali amesema, baraza limeshangazwa na hatua hiyo ya Tanesco wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaweka mkazo katika kukuza uchumi kwa kufufua na kujenga viwanda ambavyo vitategemea zaidi upatikanaji wa umeme wa uhakika katika uendeshaji wa shughuli zake za kazi.

Mariam Majimengi wa Mwenge, Dar es salaam amesema kuwa, hatua hiyo itaumiza wengi kutokana na bei hiyo kwenda sambamba na kupanda kwa bei ya bidhaa.

“Umeme unapopanda bila shaka vitu vingine vyote vitapanda. Mfanyabiashara hawezi kuongezewa gharama halafu yeye asiongeze gharama kwa mnunuzi,” amesema huku akibeba maoni ya wananchi wengi.

error: Content is protected !!