January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Muhimbili yaboresha huduma za wagonjwa wa nje

Spread the love

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imeboresha huduma za afya kwa wagonjwa wa nje ili wapate muda zaidi wa kutibiwa na kupata ushauri wa daktari katika kliniki mbalimbali nchini. Anaandika Regina Mkonde … (endelea).

Hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa wagonjwa, na kuwapunguzia muda wa kusubiri ili wapate huduma kwa wakati.

Dk. Raymond Mwenesano, Mkuu wa Idara ya Huduma ya Wagonjwa wa Nje katika hospitali hiyo, amesema utaratibu huu mpya utahusu wagonjwa wanaokuja kutibiwa na kuondoka, hasa wanaolipa kwa fedha taslimu.

Wengine watakaohusika na utaratibu huu ni wanachama wa Mfumo wa Taifa wa Bima ya Afya, bima mbalimbali za afya na watumishi ambao kampuni zao zina mikataba na hospitali.

Dk Mwenesano amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELKEZO) jijini Dar es Salaam.

 “Katika kliniki ambazo zimeshaanza kufanya kazi, madaktari bingwa pekee ndio watakaoona wagonjwa na si vinginevyo. Huduma hizi kwa sasa zinatolewa kila siku kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni. Kwa siku za Jumamosi huduma hutolewa kuanzia saa 3:00 hadi saa 8:00 mchana,” alisema Dk. Mwenesano

Mwenesano aliongeza kuwa kiliniki hizi zitafanyia kazi katika jengo la wagonjwa wa nje linalotazamana na jengo la wazazi na jengo la wagonjwa wa NHIF lililo karibu na eneo la Makuti.

Kwa mujibu wa Dk. Mwenesano, huduma za kliniki zilikuwa hazitolewi kwa kiwango cha kuridhisha kwa kukosekana muda wa kutosha wa kuhudumia wagonjwa.

Wagonjwa wanaopata rufaa kwenda Muhimbili wataendelea na utaratibu wa kawaida wa kuwasilisha barua za rufaa ili wapatiwe huduma.

Alisisitiza: “Kutokana na uboreshwaji huu, tunapenda kuwajulisha wananchi hasa wagonjwa wa kulipiwa bima za afya wafike kwa ajili ya kupata huduma za afya. Ni matumaini yetu msongamano utapungua na muda utapatikana wa madaktari bingwa kuwaona wagonjwa ambao hawana bima wala hawalipii huduma za matibabu.”

error: Content is protected !!