January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Muhammad Buhari Nigeria, Maalim Seif Zanzibar

Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF

Spread the love

RAI wa Nigeria wameamua kwa kura zao, kuchangua mgombea urais wanayemtaka. Tume ya Taifa ya Uchaguzi nayo imesimamia na kuthibitisha maamuzi ya wananchi na kumtangaza mshindi halali wa uchaguzi wa nchi hiyo, Jenerali Muhammadu Buhari.

Jenerali Buhari, ameingia Ikulu kupitia chama cha upinzani – Alliance Progressive Congress (APC). Alipata kura 15,424,921 dhidi ya aliyekuwa mshindani wake mkuu, Goodluck Jonathan.

 Katika uchaguzi huo, Jonathan aliyeingia katika kinyang’anyiro hicho kupitia chama cha Peoples Democratic Party (PDP), alipata kura 12,853,162.

Jonathan alikubali kushindwa. Kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, alimpigia simu mshindani wake, Jenerali Buhari na kumpongeza kwa ushindi aliopata.

Hapa nchini yupo mwanasiasa mmoja anayefanana kwa kiasi fulani na Muhammadu Buhari. Naye ni Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais Visiwani Zanzibar.

Kama ilivyokuwa kwa Jenerali Buhari aliyegombea urais wa Nigeria mara tatu bila mafanikio, ndivyo Maalim Seif alivyofanya huko Zanzibar.

Maalim amegombea urais mara ya nne bila kutangazwa mshindi. Ameanza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, mwaka 2000, mwaka 2005 na mwaka 2010. Anatarajiwa kugombea tena katika uchaguzi mkuu ujao.

Buhari aliwahi kuitawala Nigeria kwa njia ya kijeshi; kabla ya kugombea urais kwa njia ya kidemokrasia mara tatu, bila mafanikio.

Maalim Seif amewahi kuwa waziri kiongozi, kabla ya kufukuzwa katika chama alichokuwa – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kwenye miaka ya thamanini.

Kama ilivyokuwa safari ya kidemokrasia ya Rais Jenerali Buhari, naye Maalim Seif ametangaza tena nia ya kugombea urais Zanzibar, kupitia Chama cha Wananchi (CUF).

Hakuna shaka kuwa Maalim Seif atapitishwa kuwania nafasi hiyo na chama chake. Atapitishwa pia kama mgombea atakayepeperusha bendera ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), katika kinyang’anyiro hicho.

Muungano wa Ukawa unaundwa na vyama vinne vya NCCR- Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF), Chadema na National League for Democrats (NLD).

Mara zote alizogombea urais Zanzibar, Maalim Seif ametangazwa kupata kura zisizopungua asilimia 45. Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Katika uchaguzi wa mwaka 1995, CCM kilishinda kwa kupata asilimia 50.2 (kura 165,271 za urais) na CUF asilimia 49.8 (kura 163,706 za urais). Kura halali zilikuwa 328,977.

Hata chaguzi zilizofuata ushindani kati ya CCM na CUF umejidhihirisha. Kwa mujibu wa taarifa zilizo katika tovuti ya tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) mwaka 2005, Amani Abeid Karume wa CCM alishinda kwa kura 239,832 (asilimia 53.2), Maalim Seif alifuatia kwa kura 207,733 (asilimia 46.1) kati ya kura halali 450,968.

Mwaka 2010, Dk. Ali Mohammed Shein (CCM) kura 179,809 (50.1), Maalim Seif (CUF) kura 176,338 (49.1). Kura halali zilikuwa 358,815.

Mara zote alizogombea urais, Maalim Seif amepata kura nyingi zinazoshawishi imani wananchi wa Zanzibar waliyonayo kwake.

Kura nyingi anazopata Maalim Seif zinafanya kusiwe na mshangao bali shangwe pale atakapotangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao sawa tu na endapo itakuwa hivyo kwa mgombea wa CCM ambaye, kwa mujibu wa tamaduni isiyo rasmi ya kuachiana awamu ya pili ya kumalizia muhula kama ilivyotokea kwa Goodluck wa Nigeria, atakuwa Dk. Ali Mohammed Shein.

Lakini huwezi jua mambo ya kisiasa, CCM wanaweza kuamua tofauti hivyo si vyema kuwapangia cha kufanya jikoni. Vyombo vya habari vimeripoti matukio kadhaa ya kuchefusha visiwani Zanzibar lakini kiongozi wa Wazanzibari kwa nafasi yake ya makamu wa kwanza wa rais wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar na katibu mkuu wa CUF Maalim Seif mara zote amenukuliwa akisisitiza amani, utulivu, uvumilivu, kusamehe na kuziacha mamlaka husika kufanya kazi zake.

Uzanzibari huu wa Maalim Seif unamuongezea kura za kustahili kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu ujao. Zanzibar inahitaji mtu atakayeweza kuwaunganisha Wazanzibari kwa kuganga ya mbele na kuacha ya ndwele.

Eti ndugu Wazanzibari kwani kuna ubaya kuamua yaliyopita si ndwele mgange yajayo! Msisitizo ukiwekwa kwenye kampeni za staha, uvumilivu wa kisiasa usioingiliwa na dola, tume kuzitendea haki kura halali kwa kila mgombea na hatimaye kutangazwa mshindi kwa wakati na haki; Zanzibar itathibitisha kuwa ada ya mja hunena, muungwana ni kitendo.

Ni kweli nchi nyingi za Afrika zinahitaji mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiuongozi kwa kuondokana na baadhi ya viongozi waitwao ‘mizigo’ itakuwa ndoto Afrika kudumisha utulivu endapo Waafrika wataruhusu uongozi usiotakiwa na umma ndiyo uamue mustakabali wa umma.

Uzuri ni kwamba siku hizi nguvu hazisaidii, wananchi hawaburuziki tena kirahisi. Watu wamekinai kuburuzwa kama walivyoonesha madereva wa mabasi na malori walioshurutishwa na tamko la kukurupuka eti lazima wakasome kila baada ya miaka mitatu kwa sababu labda watakuwa wamesahau!

Hizi dharau kwa fani za watu na utaalamu sasa zinazidi mipaka barani Afrika.

Ushindani wa kisiasa Zanzibar utabaki kuwa mkubwa kati ya vyama vile vile, CCM na CUF.

Wagombea na vyama vingine kama mwanasiasa Hamad Rashid na chama cha ADC wataendelea kusindikiza kwa mara nyingine mwaka huu, kwenye uchaguzi mkuu Zanzibar.

Mwandishi wa makala haya ni Franklin Victor ambaye anapatika kwa simu: 0713 500 047

error: Content is protected !!