Saturday , 22 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mugabe aliishi shujaa, amekufa ‘dikteta’
Habari za SiasaTangulizi

Mugabe aliishi shujaa, amekufa ‘dikteta’

Marehemu Robert Mugabe
Spread the love
ALIYEKUWA Rais wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe (95), amefariki dunia, nchini Singapore. Rais wa sasa wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, amethibitisha kifo cha mwanasiasa huyo mashuhuri ulimwenguni. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Rais Mnangangwa amesema, mtangulizi wake huyo aliyeongoza Zimbabwe kutoka 1980 mpaka 2017, alipong’olewa madarakani, amekutwa na mauti nchini Singapore, alikokuwa anapatiwa matibabu.

Mugabe alizaliwa katika koloni la Uingereza la Rhodesia (Zimbabwe ya sasa), tarehe 21 Februari 1924, kutoka mtoto wa fundi seremala na miongoni mwa kabila la wengi la Washona.

“Kamarada Mugabe alikuwa ni mwanga wa mapinduzi, mwana umajui wa Afrika ambaye aliyatoa maisha yake katika ukombozi na kuwawezesha watu wake. Mchango wake kwa taifa letu na bara la Afrika hautasahaulika…” ameeleza Rais Mnangagwa.

Naye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amesema amesikitishwa na taarifa ya kicho cha aliyemuita, “Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe, Mzee Robert Mugabe.”

Amesema, “Afrika imepoteza mmoja wa viongozi jasiri, shupavu, mwanamajumui wa Afrika na aliyekataa ukoloni kwa vitendo. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.”

Kwa upande wake, rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametuma salamu za rambirambi akisema hana maneno ya kutosha kuelezea uzito wa kuachwa na kiongozi shupavu, shujaa na mzalendo wa Afrika ambaye alitekeleza jukumu muhimu katika kutetea maslahi ya bara la Afrika.

Amesema, “kwa wakati huu wa majonzi, mawazo na maombi yangu ni kwa jamaa, ndugu na watu wa Zimbabwe ambao kwa miaka mingi aliwatumikia kwa kujitolea na kwa bidii…

“Bila shaka, tutamkumbuka Rais huyo wa zamani Robert Mugabe kama mtu jasiri ambaye kamwe hakuogopa kuelezea msimamo wake kwa jambo lolote hata kama wengi hawakumuunga mkono. Kwa familia yake, Serikali na raia wa Zimbabwe, Mola awafariji na ailaze roho ya Rais wa zamani Robert Mugabe mahala pema peponi.”

Robert Mugabe, mtu ambaye alitukuzwa kama mshindi katika mapigano ya Afrika kwa kuushinda ukoloni, amefariki dunia akiwa dikteta. Alituhumiwa kwa ukikiukaji wa haki za binadamu na kuigeuza nchi ambayo ilikuwa yenye utajirimkubwa kuwa masikini wa kutupwa.

Alipa masomo yake kwa msaada wa Kanisa Katoliki na akahitimu kuwa mwalimu. Alishinda nafasi ya masomo katika chuo cha Fort Hare huko Afrika Kusini, alikopata shahada yake ya kwanza kati ya saba kabla hajaelekea nchini Ghana kufundisha.

Akiwa huko, Mugabe alivutiwa sana na fikra za kiafrika na Kwame Nkurumah. Hata mke wake wa kwanza, Bi. Sally alikuwa ni kutoka Mghana.

Mwaka 1960, Mugabe alirudi Rhodesia, na kwanza alianza kazi katika harakati za ukombozi wa Afrika na Joshua Nkomo kabla hajawa mwazilishi wa chama cha ZANU.

Mwaka 1964, baada ya kutoa hotuba yake na kuwaita waziri mkuu wa Rhodesia na serikali nzima ”Cowboys” Mugabe alikamatwa na kutupwa jela kwa miaka 10 bila ya kufunguliwa mashtaka kwa kuukosoa uongozi wa Rhodesia.

Mwaka 1973, yungali gerezani alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Zimbabwe African Union (ZANU), ambacho alikuwa ni mwanachama mwanzilishi. Mtoto wake wa kwanza alikufa akiwa gerezani na alizuiwa kwenda kumzika.

Baada ya kuachiwa kutoka gerezani, alikimbilia Msumbiji na kuongoza mapambano ya kijeshi ya kudai uhuru.

Licha ya kuwa mpiganaji wa vita vya kushtukiza, alisifika kwa kuwa mzuri kwenye majadiliano.

Mwaka 1980 akafanikiwa kuingia madarakani baada ya uchaguzi uliomaliza utawala wa walowezi wachache wa kizungu.

Kama waziri mkuu wa kwanza wa Zimbabwe na baadae rais, Robert Gabriel Mugabe alihidi kuleta Amani na usuluhishi.

Lakini matumaini yaliyoleta uhuru mwaka 1980 yakasababisha migogoro, rushwa na kuanguka kwa uchumi.

Rais Mugabe akawa mkosoaji mkubwa wa nchi za Magharibi, sana ikiwa Uingereza nchi iliyotawala Zimbabwe na aliita ni nchi adui.

Mbali na mkono wake wa chuma kwa viongozi wa upinzani na jinsi alivyokuwa akiendesha uchumi bado baadhi ya viongozi wa Afrika waliendelea kumuunga mkono.

Chama chake cha ZANU kiliungana na umoja wa Afrika Zimbabwe ama ZAPU.

Wakati wa makubaliano ya uhuru wa Rhodesia alionekana kuwa kiongozi mkakamavu wa Kiafrika na mwenye mahitaji yasiyopingika.

Alitembelea London mwaka 1976 na kusema kuwa uhuru kwa watu wa Zimbabwe, hauwezi kupatikana nje ya mtutu wa bunduki.

Namna yake ya kufanya majadiliano ilimletea heshima kwa wakosiaji wake, vyombo vya habari vilimsifia kama mwanamapinduzi mwenye kufikiri.

Mwaka 1979 yalifikiwa makubaliano ya kuicha huru na kutengenezwa kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe na Februari 1980, uchaguzi wa kwanza wa serikali mpya ulifanyika.

Uchaguzi ulimalizika kwa ushindi mkubwa sana kwa Mugabe ingawa kulikua na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu, ZANU ilipata ushindi wa kutosha.

Ushindi wa Mugabe ulimaanisha Wazungu wengi waanze kufunga mizigo yao tayari kwa kuondoka Rhodesia, wakati wafuasi wake wakicheza mitaani.

Lakini hotuba zake za mwanzo ziliweka mambo sawa, Mugabe aliahidi serikali yenye ushirikiano, kusingekuwa na namna yoyote ya kutaifisha mali binafsi, lengo lake alisema litakua ni makubaliano.

Baadaye mwaka huo, alitoa sera yake ya kiuchumi, ikiwa na mchanganyiko wa biashara kati ya serikali na sekta binafsi.

Wakati huo waziri mkuu Nkomo alikuwa akisisitiza utawala wa chama Kimoja. Uhasama baina yake na Mugabe ukaongezeka.

Baada ya kugundulika kwa mali kufichwa zinazomilikiwa na ZAPU, Nkomo na wenzake walipunguzwa na wakaondolewa serikalini.

Wakati akiendela kubana demokrasia, Mugabe alihakikisha wapinzani wake hawapumui vizuri.

Katikati ya mwaka 1980 yalifanyika mauaji ya maelfu ya wafuasi wa Nkomo kutoka kabila la Ndebele eneo la Matabaleland.

Mugabe alihusishwa na mauaji hayo ambayo yalitekelezwa na kundi la jeshi lilipata mafunzo Korea Kaskazini, lakini hakuchukuliwa hatua zozote.

Kwa msukumo mkubwa Nkomo alilazimishwa kukubali chama cha cha ZAPU kuungana na ZANU na kuwa chama kimoja kikubwa ZANU-PF.

Baada ya kuvunjwa kwa ofisi ya waziri mkuu, Mugabe akawa rais tena 1987 na kisha akashinda tena muhula wa tatu mwaka 1996.

Mwaka huo huo akamuoa mkewe Grace Marufu, baada ya mke wake wa kwanza kufariki kwa ugonjwa wa kansa.

Mugabe alikua tayari na watoto wawili na watatu akazaliwa wakati mugabe akiwa na miaka 73.

Alipata mafanikio ya kuweka jamii isiyo na ubaguzi, lakini mwaka 1992 alitambulisha sheria ya ardhi ambao ilipelekea ubinafshwaji wa adhri bila kukata rufaa.

Mpango huo, ulilenga kupokonywa ardhi ya zaidi ya wakulima wa kizungu 4,500 ambao walikua wakimiliki maeneo mazuri ya nchi hiyo.

Mapema mwaka 2000, huku uraisi wake ukiwa katika mashaka baada ya kuundwa kwa chama kipya cha MDC kilichoongozwa na kiongozi mwenzake wa zamani wa vyama vya wafanyakazi, Morgan Tsvangirai, Mugabe akawaondoa wakulima.

Wafuasi wake waliokua wakijiita ”mashujaa wa kivita,” walivamia maeneo hayo yaliyomilikiwa na wazungu, baadhi wa wakulima waliuawa na wafanyakazi wao weusi.

Suala hili lilisababisha uchumi wa Zimbabwe uzidi kudidimia, wakosoaji wa Mugabe walilalamika kuwa kitendo chake kimesababisha uharibifu.

Zimbabwe ikaporomoka haraka sana kutoka kuwa moja ya nchi zenye uchumi mkubwa hasa katika kilimo hadi kutegemea misaada kulisha wananchi wake.

Uchaguzi wa mwaka 2000 wa wabunge, MDC ilishinda viti 57 kati ya 120 huku viti 20 vikashikiliwa na walioteuliwa na Mugabe.

Miaka miwili baadae, katika uchaguzi wa Urais, Mugabe alipata asilimia 56.2 dhidi ya mpinzani wake Tsvangirai aliyepata asilimia 41. 9; idadi kubwa ya watu maeneo ya vijijini walipata vikwazo kwenye kupiga kura kutokana na vituo vya kupigia kira kufungwa.

wafuasi wa MDC walivamiwa nchi nzima mwaka 2018, pamoja na Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya hawakutambua matokeo ya uchaguzi kutokana na vurugu lakini pia malalamiko ya wizi wa kura.

Mugabe na Zimbabwe ikazidi kutengwa na mataifa ya nje. Jumuiya ya madola pia ilizuia Zimbabwe kushiriki mikutano yake hadi pale demokrasia itakaporudi.

Mwezi wa tano mwaka 2015, Mugabe alitambulisha operesheni ya kuleta amani na kuondoa biashara haramu.

Wafanyabiashara ndogo ndogo za mtaani zaidi ya 30,000 walikamatwa na vibanda vyao kubomolewa na kuacha zaidi wa wazimbabwe 70,000 wakiwa hawana makazi.

Mwezi machi 2008, Mugabe alishindwa katika awamu ya kwanza ya uchaguzi wa uraisi, ingawa baadae mwezi Juni, alishinda baada ya mpinzani wake Tsvangirai kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Baada ya ushindi huo, Tsvangira alieleza kwamba, ni vigumu kuwa na uchaguzi huru na wa haki nchini humo.

Uchumi wa Zimbabwe uliendelea kushuka huku bei ya bidhaa ikiongezeka maradufu.

Baada ya watu kuanza kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa kipindupindu kufuatia serikali kushindwa kugharamia kutibu maji kwa kutumia kemikali raisi Mugabe alifiakiana na adui zake wa muda mrefu kushiriki madaraka.

Makubaliano ya kushiriki uongozi yalizuia utata, baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo, hatimaye mwezi Februari 2009 bwana Tsvangirai aliapishwa kuwa waziri mkuu wa Zimbabwe.

Haikuwa ni kitu cha kushangaza pamoja na mabadiliko yaliyofanywa kutokana na mzozo na mashitaka ya mara kwa mara kutoka kwa taasisi za haki za binadamu kuwa wapinzani wa kisiasa wa Mugabe walikuwa wakikamatwa na kuteswa.

Sifa ya bwana Tsvangirai pia ilishuka kutokana na kujihusisha na utawala wa Mugabe kama waziri mkuu pamoja na kuwa hakuwa na nguvu kwenye utawala huo.

Kwenye uchaguzi mkuu 2013 ambao Rais Mugabe alishinda kwa asilimia 61 ya kura zote, alivunja makubaliano ya kuchangia madaraka na bwana Tsvangirai katikati ya malalamiko ya wizi wa kura.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-Moon aliingilia kati kutaka uchunguzi ufanyike. Kwa kipindi hicho hakuna machafuko makubwa yaliyotajwa katika chaguzi zilizofanyika nchini Zimbabwe.

Kwa kadiri miaka yake ilivyozidi kuongezeka huku na matatizo ya kiafya pia yakizidi kuongezeka yalileta minong’ono ya nani wa kuichukua nafasi yake.

Lakini fitna ziliendelea kufanyika kwa wale walioonekana wanaweza kuchukua nafasi ya yake na hivyo kuthibitisha namna uongozi wa Zimbabwe unashikiliwa na Mugabe pekee.

Na hata Mugabe alionekana kuvunja nguvu ya utawala wowote uliokuwa kinyume nae.

Kufuatia uvumi wa mkewe Grace kutaka kutawala pale mume wake atakapofariki akiwa madarakani, Mugabe alitangaza nia yake ya kugombea tena mwaka 2018 ambapo angekuwa na umri wa miaka 94.

Na katika kuondoa maswali yaliyokuwa yamebaki kati ya wale waliokuwa wakidhaniwa huenda wangekuwa warithi, mwezi Februari, Mugabe alitangaza rasmi kuwa ataendelea kuwa madarakani mpaka pale Mungu atakapomuita.

Kufuatia tukio hilo, haikuwa tena Mungu ila ni umoja wa majeshi wa Zimbabwe ndiyo yaliyomuita Mugabe. Novemba 2017 aliwekwa kizuizini kwa siku nne huku aliyekuwa makamo wake Emmerson Mnangagwa akichukua nafasi yake kama kiongozi wa Zanu-PF.

Novemba 21 spika wa bunge la Zimbabwe alitangaza rasmi kujiuzulu kwa raisi Mugabe baada ya muda mrefu kukataa kibabe kufanya uamuzi huo.

Mugabe alifikia makubaliano ya kupata ulinzi kwake na familia yake kutokana na hofu ya kuuawa na kuendeleza biashara yake. Pia alipatiwa nyumba, wafanyakazi, usafiri na hadhi yake ya kidiplomasia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Askofu Wolfang Rais mpya TEC, Padri Kitima aula tena

Spread the loveBARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetambulisha safu mpya za...

Habari MchanganyikoTangulizi

Padre anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe, asimamishwa

Spread the loveKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yaahidi kushirikiana na Prof. Ndakidemi kuhamasisha zao la kahawa

Spread the loveSerikali imeahidi kuungana na Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

IMF yaimwagia Tanzania trilioni 2.4 kukabili mabadiliko ya hali ya hewa

Spread the loveShirika la Kimataifa la Fedha (IMF) jana Alhamisi limesema bodi...

error: Content is protected !!