
Sheikh, Mkuu, Mufti Issa Shaaban Simba (kushoto enzi za uhai wake) na Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum
MUFTI wa Tanzania, Shaaban Issa Bin Simba, anatarajiwa kuzikwa leo mkoani Shinyanga baada ya kuagwa Jijini Dar es Salaam. Anaandika Jimmy Mfuru … (endelea).
Mufti alifariki jana asubuhi katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam ambapo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na presha.
Taarifa kutoka Makao Makuu ya Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) kupitia kwa Shekhe Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum zinaeleza kuwa, viongozi na watu mbalimbali watakusanyika makao makuu hapo na mwili wake utaagwa kuanzia saa tano asubuhi.
Akifafanua amesema, baraza limekubaliana na familia wa marehemu kuwa Mufti azikwe leo badala ya taarifa ya kwanza iliyoelekeza kuwa, atazikwa Alhamisi kwa kile alichosema kuwa agizo la Mufti ‘azikwe haraka.’
“Baraza limekubaliana na familia ya marehemu Mufti azikwe leo mkoani Shinyanga baada ya kuagwa jijini Dar es Salaam,” amesema Shekhe Salum.
Sheikh Alhad akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya taasisi hiyo Kinondoni, amesema Mufti Simba kabla ya kifo chake alikuwa ametoka kwenye safari zake za kikazi mikoani.
Shekhe Simba alichaguliwa kuwa Mufti wa Tanzania mwaka 2002 uchaguzi ambao ulifanyika kutokana na kifo cha mtangulizi wake Sheikh Hemed Bin Juma.
Kinyang’anyiro cha kumpata Mufti mwaka 2002 kilikuwa kikali ambapo walikuwa wakichuana yeye (Mfufti Simba) na Marehemu Sheikh Suleiman Gorogosi.
Mufti Simba alizaliwa wilayani Magu katika Mkoa wa Mwanza mwaka 1937. Kabla ya kuchaguliwa kuwa Mufti, alikuwa Sheik Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Kwa mujibu wa Katiba ya BAKWATA, Mufti anapofariki dunia, utaratibu wa kujaza nafasi yake hufanywa baada ya siku 90. Wakati nafasi hiyo inasubiriwa kujazwa, hukaimiwa na mjumbe mmoja wa Baraza la Maulamaa ambaye ni Kadhi Mkuu, Sheikh Abdallah Mnyasi.
More Stories
IGP Sirro: Hatufungui kesi za madai, migogoro ya ardhi
Panyabuku waanza kubaini TB
Kigogo wa KKKT Kaskazini afariki dunia