January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mufti Simba afariki, viongozi wamlilia

Mufti Issa Shaaban Simba enzi za uhai wake

Spread the love

MUFTI wa Tanzania, Shaaban Issa Bin Simba, amefariki dunia leo saa 1:30 asubuhi katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Taarifa kutoka Makao Makuu ya Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA), zinaeleza kuwa, Mufti Simba alikuwa akisumbuliwa na presha, kisukari pamoja na mapafu.

Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya taasisi hiyo, amesema, Mufti Simba kabla ya kifo chake alikuwa ametoka kwenye safari zake za kikazi mikoani.

“Alikuwa mkoani katika safari ya kikazi na aliporejea alikuwa hajisikii vizuri ndipo tukampeleke katika Hospitali ya TMJ,” amesema Alhad na kuongeza;

 “Alikuwa akisumbuliwa na maradhi yake ya kawaida ambayo ni presha na kisukari lakini baada ya kutoka mikoani ndio akawa anashindwa kupumua vizuri,” anasema na kwamba, ndipo walipompelekea Hospitali ya TMJ kwa matibabu na baadaye kufariki dunia.”

Kuhusu maziko, Alhad amesema, taarifa za awali Mufti Simba alikuwa azikwe nyumbani kwao Shinyanga Alhamisi wiki hii na kwamba, taarifa hizo zinaweza kubadilika kutokana na mke wa marehemu kueleza wosia wa Mufti kwamba “akifariki azikwe haraka.”

Alhadi amesema, familia na viongozi wengine wanaendelea kujadili kauli hiyo na ile ya awali ya kuzikwa Alhamis na baadaye kutoa uamuzi wa pamoja.

“Kuna kauli mbili na zote zina nguvu, mama (mke wa Mufti) na ile ya awali ya kuzikwa Alhamis. Tunaendelea na kikao ili kujua nini tufanye, hizi ndio taarifa za sasa na taarifa zaidi zitafuata,” Alhad amewaambia waandishi.

Hata hivyo, amesema, pamoja na kuwa Mufti atazikwa Shinyanga, Watanzania na Waislamu wote kesho watajumuika kumwombea marehemu katika viwanja vya ofisi hizo zilizopo Kinondoni “kwa kuwa si kila mtu anaweza kwenda Shinyanga kushiriki mazishi.”

Amiri wa Shura ya Maimamu nchini, Shekh Mussa Kundecha amesema, Mufti Simba ni moja wa viongozi watakaokumbukwa kwa mambo mengi nchini.

Amesema kuwa, ameongoza taasisi hiyo kwa namna ambavyo aliweza kukabiliana na changamoto mbalimbali ndani ya taasisi hiyo.

“Ndani ya BAKWATA kuna changamoto mbalimbali kama ilivyo taasisi nyingine zote nchini, kwa hakika kajitahidi kwa namna yake kukabiliana na changamoto hizo na BAKWATA kuendelea kuwepo kama ilivyo,” amesema Sheikh Kundecha.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye ametuma salamu za rambirambi kwa Waislam nchi kutokana na kifo cha Mufti Mkuu Simba akisema, atakumbukwa kwa namna aliyosimama kama kiongozi wa dini.

Mbowe amesema, Mufti Simba kupitia kauli zake mara kwa mara alikuwa akisisitiza ushirikiano ndani ya jamii ya Watanzania bila kujali tofauti zao katika itikadi za dini.

“Mara kwa mara Mufti Mkuu Simba amesikika akiwaambia Watanzania, si Waislam pekee aliokuwa akiwaongoza kiroho, hata wale wanaoamini katika madhehebu tofauti, umuhimu wa kudumisha ushirikiano miongoni mwa dini mbalimbali na makundi mengine katika jamii ikiwa ni mojawapo ya misingi ya kuimarisha umoja wa taifa letu.

“Naungana na Waislam wote nchini katika wakati huu wa kuomboleza kifo cha kiongozi huyu wa kiroho. Kwa niaba ya uongozi wa Chadema, wanachama, wapenzi na wafuasi, natoa salaam za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, BAKWATA, viongozi wa kiroho nchini na Watanzania wote ndani na nje ya nchi walioguswa na msiba huu mzito,” amaesema Mbowe.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mkangara pia ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Mufti Simba na kuongeza kuwa, ni jambo la kusikitisha kumpoteza kiongozi huyo katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Mukangara amesema, Mufti Simba ameshirikiana vizuri na viongozi wote wa dini na serikali kwa kusisitiza amani nchini “na katika hili atakumbukwa kwa upole na ukarimu wake”.

error: Content is protected !!