April 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mufti Aboubakar atoa msimamo ndoa chini ya miaka 18 

Aboubakar Zubeir, Mufti wa Tanzania

Spread the love

MUFTI wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir ametoa msimamo kuhusu ndoa chini ya miaka 18, kwamba Uislam unatazamia baleghe. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akizungumza baada ya kongamano maalum la viongozi wa dini kuelekea uchaguzi jana tarehe 28 Oktoba 2019 alisema, kwa maslahi ya elimu kwa mtoto wa kike, anapaswa kuendelea na masomo yake.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba kama binti huyo amebaleghe na haendelei na masomo na anaelekea kufanya ufisadi, kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislam, binti huyo ataozeshwa.  

“Ni vizuri akaendelea kupata elimu inayomjenga,” amesema Mufti Zubeir na kuongeza “lakini kama hakuna jambo lolote linaloendelea kwake, hawezi kuachwa akae tu mpaka afikishe miaka 18 huku anafanya ufisadi, ikifikia suala la namna hiyo, apate mume aolewe.”

Mufti Zubeir ametoa msimamo huo baada ya kuulizwa na wanahabari kuhusu hukumu ya Mahakama ya Rufaa tarehe 23 Oktoba 2019, kuridhia hukumu ya Mahakama Kuu ya kubatilisha vifungu vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971, vinavyoruhusu binti chini ya miaka 18 kuolewa.

Rebecca Gyumi ambaye ni mwanaharakati na mkurugenzi wa shirika lisilo la Kiserikali la Msichana Initiative, ndiye aliyejenga hoja ya kutaka kutenguliwa kwa kifungu hicho, akidai kinakiuka Katiba ya Jamhuri na kumnyima mtoto wa kike haki ya kupata elimu.

Awali, Mahakama Kuu ilitoa hukumu kwamba ni kinyume cha sheria binti chini ya miaka 18 kuolewa, hata hivyo serikali ilikata rufaa ya hukumu hiyo katika Mahakama ya Rufaa. Mpaka sasa serikali haijatoa tamko kufuatia rufaa yake kushindwa.

Katika rufaa hiyo iliyosomwa na Naibu Msajili, Eddie Fussi imesema kuwa, Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kuamua kuwa vifungu hivyo ni vya kibaguzi kati ya mtoto wa kike na wa kiume, na havina manufaa yoyote kwa mtoto wa kike.

error: Content is protected !!