July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mtumishi wa Jiji Mwanza atuhumiwa kutapeli

Spread the love

ANGELINA Mabula, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza uongozi wa Jiji la Mwanza kumkamata Asubuhi Otieno, aliyekuwa Ofisa Ardhi wa jiji hilo kwa madai ya utapeli wa kiwanja, anaandika Moses Mseti.

Otieno ambaye kwa sasa amehamishiwa mkoani Mara anatuhumiwa kwa utapeli wa kiwanja kimoja kilichopo Nyakato jijini hapa mali ya Neema Paulo.

Pia anatuhumiwa kwa kosa la kumtapeli Neema Paulo Sh. 40,0000 kwa madai ya kumlaghai kuwa ni za kupimia kiwanja chake.

Madai hayo yaliibuliwa jana katika kikao kilichowahusisha Watumishi wa Idara ya Ardhi, Adam Mgoyi ambaye ni Mkurugenzi wa Jiji hilo pamoja na wananchi wengine waliokuwa na kero nyingi za ardhi.

Waziri huyo amesema kuwa, Otieno anapaswa kurejeshwa jijini humo kwa lengo la kujibu tuhuma hizo na kwamba ikibainika amehusika na utapeli huo afunguliwe shauli mahakamani.

Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani hapa amesema, kitendo cha mtumishi huyo kufanya utapeli kinaendelea kuitia doa serikali hivyo.

“Lugha yenyewe iliyoandikwa hapa imeandikwa kwa kiingereza na hii inawezekana ndio tatizo, haiwezekani uchukue fedha za mtu kwa lengo la kumpimia eneo lake, halafu ugeuze kibao ionekane yeye ndie kauza,” amesema Mabula.

Akizungumza huku akitokwa na machozi, Neema Paulo amesema kuwa, alitoa fedha hizo kwa lengo la kupimiwa kiwanja chake lakini cha kushangaza baada ya miezi sita alipelekewa barua ilimtaka kuondoka katika kiwanja hicho.

Amesema, katika barua hiyo ilionesha kwamba ameuza kiwanja chake kwa Sh. 40,0000 kwenda kwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Thobias Andrew hivyo anatakiwa kuondoka katika eneo hilo.

“Nilitoa fedha zangu kwa ajili ya kupimiwa eneo, kumbe zile hela nilizotoa ndizo waliandika kwamba nimepewa na Thobias Andrew, mimi waziri nakuomba unisaidie (Naibu Waziri Angelina Mabula),” amesema Paulo.

error: Content is protected !!