Saturday , 20 April 2024
Home Kitengo Habari Kimataifa Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda akamatwa Afrika Kusini
KimataifaTangulizi

Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Fulgence Kayishema
Spread the love

 

MMOJA wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya Kimbari ya Rwanda (1994), Fulgence Kayishema, amekamatwa nchini Afrika Kusini, baada ya msako wa zaidi ya miaka 20. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

 Vyanzo mbalimbali vya taarifa kutoka mashirika ya kimataifa ya habari, ikiwamo BBC, zinaeleza kuwa Kayishema, alikamatwa jana Jumatano katika mji wa Paarl, katika operesheni ya pamoja kati ya mamlaka za Afrika Kusini na timu ya Umoja wa Mataifa (UN).

Kulingana na shirika la UN linaloshughulikia kesi bora za uhalifu wa kivita kwa Rwanda na Yugoslavia – International Residual Mechanism for Criminal Tribunals’ (IRMCT) – Kayishema alikuwa mmoja wa watu waliotoroka baada ya kutenda uhalifu wa mauaji ya Kimbari na ambao wamekuwa wakitafutwa kwa udi na uvumba.

Alishtakiwa mwaka 2001 na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), kwa makosa mbalimbali, ikiwamo mauaji ya halaiki, kushiriki katika mauaji ya halaiki, kula njama ya kutekeleza mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu, pamoja na mauaji na uhalifu mwingine.

Anatuhumiwa kupanga mauaji ya takribani Watutsi 2,000 – wanawake, wanaume, watoto na wazee – katika kanisa moja lilipo wilayani Kivumu, ambapo alikuwa inspekta wa Polisi.

Aidha, Kayishema anatuhumiwa kushiriki moja kwa moja katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo, ikiwa ni pamoja na kununua na kusambaza petroli ili kuchoma kanisa hilo pamoja na waliokuwa wanatafuta hifadhi katika nyumba hiyo ya ibada.

“Hili liliposhindikana, Kayishema na wenzake wengine, walitumia tingatinga kuangusha kanisa, kuwazika na kuwaua wakimbizi waliokuwemo ndani yake,” inaeleza sehemu ya hati yake ya mashitaka.

Kisha Kayishema na wenzake, “walisimamia uhamishaji wa maiti kutoka katika viwanja vya kanisa hadi kwenye makaburi ya pamoja kwa takriban siku mbili zilizofuata,” taarifa ya IRMCT imeeleza.

Mshukiwa ambaye amekuwa akitoroka tangu kufunguliwa mashitaka, anatazamiwa kufikishwa katika mahakama ya Cape Town siku ya Ijumaa, ripoti zinasema.

Takriban watu karibu 800,000 waliuawa pale waasi wa Kihutu wenye msimamo mkali walipowauwa Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa kati, katika muda wa siku 100, kuanzia kuuliwa kwa marais Juvenal Habyarimana wa Rwanda na Cyprien Ntaryamira wa Burundi tarehe 6 Aprili hadi katikati ya Julai 1994.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!