August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mtuhumiwa ukatili Z’bar anaswa

Omar Said Omar

Spread the love

OMAR Said Omar, mwenye umri wa miaka 24, ambaye anatuhumiwa kumchoma moto mwanamke anayefanyakazi hoteli ya kitalii Zanzibar na ambaye anatajwa kuwa ni mpenzi wake, amekamatwa akijaribu kutoroka, anaandika Jabir Idrissa.

Kijana huyo alikamatwa na polisi jana mchana eneo la Mkunazini, karibu na kituo kidogo cha polisi kwa Khamis Machungwa, Mkunazini, mjini Zanzibar, akiwa ndani ya gari katika mazingira yanayohofiwa kuwa alikuwa akijaribu kutoroka mkono wa sheria.

Kukamatwa kwake kunakuja wakati mwanamke anayetajwa kumhujumu aitwae Samira Abbas (23), akiugulia majeraha makubwa kwenye Hospitali ya Makunduchi, yenye hadhi ya hospitali ya mkoa, wilaya ya Kusini, Unguja.

Habari za kipolisi zimeeleza kuwa Samira, msichana mwenye wazazi wake wilayani Kibaha, amepata majeraha kutokana na kuchomwa moto na mtuhumiwa ambaye vyanzo vya habari vinamtaja kama mpenzi wake aliyemtuhumu kwa usaliti.

Samira ameajiriwa na hoteli ya kitalii iliyoko ukanda wa kitalii wa Kusini – East Coast Tourism Zone – ndani ya kisiwa cha Unguja. Anaishi kijiji cha Paje, Wilaya ya Kusini.

Taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP Hassan Nassir Ali, zimesema Omar alikamatwa akiwa ndani ya gari ikipita penye makutano ya barabara inayotokea Mnazimmoja hadi Bandarini Malindi na inayotokea ng’ambo upande wa Michenzani.

Mwandishi mmoja wa habari aliyeko mjini Zanzibar, ameiambia MwanaHalisiOnline kuwa mtuhumiwa alikamatwa baada ya polisi waliofika eneo hilo kulazimika kufyatua risasi za mipira ili kutawanya kundi la wananchi waliofika haraka hapo baada ya kusikia kugundulika kwa mtuhumiwa akikimbilia bandarini.

“Labda wanaomfuatilia waliamini anakimbilia bandarini kupanda boti ya kwenda jijini Dar es Salaam kwa nia ya kujificha. Kamanda wa Polisi ametoa taarifa kwamba mtuhumiwa hatimaye amekamatwa,” amesema mwandishi huyo.

ACP Nassir amekaririwa akisema mtuhumiwa alikamatwa kutokana na msako mkali ulioanzishwa na kikosi cha kudhibiti uhalifu Mkoa wa Mjini Magharibi, kushirikiana na wapelelezi wa Mkoa wa Kusini Unguja, baada ya kupatiwa taarifa kuhusu tukio analohusishwa nalo.

“Askari walijitahidi vya kutosha kumtaka dereva wa gari asimame kwa amani lakini alibisha na kuongeza mwendo wa gari. Bila ya shaka dereva alimsaidia mtuhumiwa kukimbia. Kwa hivyo askari wakalazimika kupiga risasi wakilenga matairi ambayo yalitobolewa na dereva kushindwa kuendesha na askari wetu wakamdhibiti pamoja na kumkamata mtuhumiwa Omar,” amesema ACP Nassir.

Kamanda wa Polisi amesema dereva huyo naye ataunganishwa kwenye kesi itakayofunguliwa kuhusu uhalifu uliohusishwa na mtuhumiwa Omar kwa kuwa alikataa amri ya kutakiwa kusimama kwa amani.

Hali ya Samira imeelezwa kuwa si nzuri, hivyo kuibua shaka kuwa upelelezi wa kesi utahitaji kujua hatima ya majeraha yake.

error: Content is protected !!