Friday , 2 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mtoto wa Mbunge Chadema aibua mjadala kesi ya Mbowe, wenzake
Habari za Siasa

Mtoto wa Mbunge Chadema aibua mjadala kesi ya Mbowe, wenzake

Spread the love

MTOTO wa mbunge wa Chadema katika jimbo la Tarime Mjini, Easter Matiko, ameibua mjadala kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kufuatia mama yake huyo mzazi kutotokea mahakamani. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Matiko, ni miongoni mwa viongozi wandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, wanaokabiliwa na kesi ya jinai katika mahakama hiyo.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri, wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, leo tarehe 2 Agosti, ameiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka hauna taarifa za kutokuwepo mbele ya mahakama kwa mtuhumiwa namba tano katika kesi hiyo – Easter Matiko.

Awali kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala, ameieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo amepata dharula ya haraka ya kutakiwa afike shuleni kwa mtoto wake mjini Nairobi nchini Kenya.

Kibatala aliiomba mahakama imruhusu mdhamini wa wake, Patric Assenga, ambaye ni diwani wa kata ya Tabata, eleze dharula aliyopata mdhamana wake.

Asenga alisema, alipewa taarifa na mdhamana wake (Matiko), kuwa jana usiku alipigiwa simu kutoka katika shule anayesoma mtoto wake jijini Nairobi kuwa anatakiwa kufika haraka kuna dharula juu ya mtoto wake.

Baada ya kueleza hayo, wakili Nchimbi ameleza kuwa ana mashaka na kinachoitwa, “dharula ya Matiko,” kwa kuwa hata mawasiliano kati yake na mdhamini wake (Asenga), ambayo yaliyowasilishwa mahakamani, yanaonesha kuwa yaliyafanyika leo saa 3 asubuhi.

“Kama angekuwa ameondoka jana, kama inavyoelezwa, hadi muda huo angeweza kueleza sababu ya kuitwa ghafla shuleni Niarobi,” alieleza Nchimbi.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mashauri alimtaka Asenga kufuatilia kilichosababisha Matiko kuondoka ghafla kuelekea Nairobi.

Aidha, Nchimbi aliomba mahakama kupanga usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo, kufanyika tarehe 6 Agosti.

Hata hivyo, Kibatala alitaka mahakama kupanga siku nyingine kwa madai kuwa tarehe iliyopendekezwa na wakili wa serikali, inakinzana na ratiba yake.

Alisema, siku hiyo atakuwa kwenye Makama Kuu kusikiliza rufaa ya marejeo katika shauri ambalo limefunguliwa na watuhumiwa.

Kibatala akataja pia siku inayofuata, tarehe 7 Agosti kuwa na mashauri mengine Mahakama Kuu; huku tarehe 8 Agosti, akiielezea kuwa mtuhumiwa namba mbili, Peter Msigwa, atakuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, mkoani Iringa, kusikiliza kesi zinazomkabili.

Baada ya ubishani huo, Hakimu Mashauri, alipanga  tarehe 6 Agosti, kuwa utafanyika usikilizwaji wa awali.

Katika kesi hiyo, mbali na Matiko na Msigwa,  waoshitakiwa wengine, ni pamoja na Freeman Mbowe,  Dk. Vicent Mashinji, Halima Mdee, John Mnyika na Easter Bulaya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Lusinde: CCM hatuliachii ng’o jimbo la Moshi Mjini

Spread the loveMJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Livingston...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar: Bakharesa hajavamia shamba letu

Spread the love  IKULU Visiwani Zanzibar, imeeleza kuwa eneo la kiwanda cha...

Habari za SiasaTangulizi

Zanzibar watangaza rasmi kuwa shamba la Razaba ni mali yao

Spread the love  SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetangaza rasmi kwamba shamba...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Mwinyi azindua Kamati ya Maridhiano Visiwani

Spread the love  RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Hussein...

error: Content is protected !!