FREDRICK, mtoto wa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amechukua fomu ya kugombea ubunge Monduli, mkoani Arusha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Fredrick amechukua fomu hiyo leo Jumanne tarehe 14 Julai 2020, katika Ofisi za CCM wilayani Monduli, mkoani Arusha na kukabidhiwa na Katibu wa chama hicho Wilaya ya Monduli, Langael Akyoo.
Mtoto huyo wa Lowassa amechukua fomu hiyo ili kujaribu bahati ya kuliongoza jimbo hilo, lililokuwa mikononi mwa baba yake tangu mwaka 1990 hadi 2015.
Lowassa aliliongoza jimbo hilo katika vipindi vitano mfululizo, kupitia Chama cha CCM.
Mwaka 2015 baada ya kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na kugombea urais na kuungwa mkono na vyama vya CUF, NLD na NCCR-Mageuzi vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jimbo hilo lilikwenda upinzani.
Julius Kalanga alishinda ubunge kupitia Chadema. Hata hivyo, usiku wa tarehe 31 Julai 2018 alijiuzulu ubunge na kuhamia CCM ambako alipitishwa tena kuwania ubunge na kushinda.
Leave a comment