November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mteule wa JPM atuhumiwa kuomba rushwa, ni DC wa Hai

Lengai Ole Sabaya, Mkuu wa Wilaya ya Hai

Spread the love

LENGAI Ole Sabaya, Mkuu wa Wilaya ya Hai (DC) anatuhumiwa na Carthbert Swai, mfanyabiashara na Mmiliki wa Hoteli ya Kitalii ya Weruweru River Lodge, kumwomba rushwa. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Katika mkutano wa kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika tarehe 22 Julai 2019, Swai alidai, Sabaya alimpa vitisho akimtaka ampe fedha kiasi cha Sh. 5 milioni.

Vile vile, mfanyabaishara huyo alidai Sabaya alimuweka ndani meneja wake, akimtaka aeleze taarifa ya mapato ya hoteli yake ya Weruweru River Lodge.

MwanaHALISI ONLINE lilimtafuta Swai ili kujua undani wa tuhuma hizo, simu yake ilipokewa na mewe Stella Swai ambaye alisema, mumewe ameitwa kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Kilimanjaro kuhusu tuhuma zake dhidi ya Sabaya.

“Mume wangu ameitwa Takukuru, ameshawasili katika ofisi hizo Mkoa wa Kilimanjaro. Ameitwa kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu tuhuma alizotoa kwenye mkutano wa Kamishna wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro na wafanyabaishara wa mkoani hapa,” amesema Stella na kuongeza:

“Swai alitoa tuhuma hizo siku ya Jumatatu katika mkutano huo. Kwa maelezo zaidi subiri akirudi ataeleza kila kitu kuhusu wito huo.”

Tarehe 22 Julai 2019, katika mkutano wa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro na wafanyabaishara wa mkoa huo, Swai alidai kwamba Sabaya alimpa vitisho akimtaka ampe fedha kiasi cha Sh. 5 milioni.

Joseph Muteci, meneja mkuu wa hoteli hiyo amesema, ni kweli Ibrahim Kapilima, meneja msaidizi wa biashara katika hoteli hiyo, aliwekwa mahabusu baada ya kushindwa kutoa taarifa za mapato za hoteli hiyo.

Muteci ameeleza, Kapilima alishindwa kutoa taarifa hizo, kwa kuwa hahusiki na masuala ya mapato ya hoteli hiyo.

“Mimi sikuwepo wakati huo, lakini ni kweli meneja msaidizi aliwekwa ndani baada ya kushindwa kutoa taarifa za mapato.

“Kwa mujibu wa kazi yake, hakuwa na uwezo wa kutoa taarifa za mapato ya hoteli. Mmiliki alifuatilia suala hilo na Kapilima alitolewa,” amesema Muteci.

MwanaHALISI ONLINE ilimtafuta DC Sabaya kutaka ufafanuzi kuhusu tuhuma dhidi yake, hata hivyo aliomba atafutwe baadaye kwa kuwa anaandaa mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa suala hilo.

error: Content is protected !!