August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mteule wa JPM aiga mbwembwe

Spread the love

KIOMONI Kibamba, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, ameanza kazi kwa kuiga mbwembwe za Hamisi Kigwangala, Naibu Waziri wa Afya, anaandika Moses Mseti.

Amefika ofisini na kisha kuwafungia geti baadhi ya watumishi wa halmashauli hiyo waliochelewa kuingia kazini kwa wakati.

Tarehe 18 Desemba mwaka huu, Dk. Kigwangala aliwafungia geti baadhi ya wafanyakazi wa wizara hiyo waliochelewa kuingia kazini.

Kibamba akizungumza na waandishi wa habari leo mara baada ya kuchukua uwamuzi wa kuwafungia nje wafanyakazi hao amesema kuwa, katika kipindi kifupi tangu awasili jijini humo amebaini kuwepo kwa watumishi wachelewaji sugu.

Amesema kuwa, baada ya yeye kufika ofisini saa 12:45 asubuhi, alishangaa kuona baadhi ya wafanyakazi wa ofisi hiyo wakiingia hadi zaidi ya saa 2:30.

Amesema kuwa, baada ya kuona hali hiyo, aliamua kufunga geti ili kujenga utamaduni wa watumishi wa umma hususani katika jiji hilo kuwahi kufika kazini kwa wakati muafaka.

Kibamba amesema, kwa mjibu wa sheria ya utumishi ya umma ya mwaka 2009, vipo vifungu vinavyoelekeza wajibu na muda wa mtumishi wa umma kufika kazini ambapo ni saa 1:30 asubuhi na hatua wanazopaswa kuchukuliwa kwa wachelewaji.

“Mtumishi wa umma anatakiwa kufika kazini saa moja na nusu asubuhi na kutoka kazini saa tisa na nusu jioni, kwa maana hiyo anapaswa kufanya kazi kwa saa nane, utakuta watu wanafanya kazi kinyume na utaratibu.

“Leo hatua nilizowachukulia ni kuwapa onyo kwa mdomo lakini kama wataendelea na uitaratibu wa kuchelewa kazini, tutawachukulia hatua nyingine zaidi kwa mjibu wa kanuni za utumishi wa umma,” amesema Kibamba.

Katika hatua nyingine Kibamba ametahadhalisha watumishi wa umma katika sekta zilizopo chini yake ikiwemo shuleni na vituo vya afya kujiandaa kutumbuliwa endapo watabainika wanachelewa kufika kazini.

Tundosa Waryama, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tawi la Mwanza (Talgwu) amesema, Kibamba amekurupuka kwa kuanza utaratibu wa kuwafungia wafanyakazi.

Waryama amesema kuwa, alichopaswa kufanya mkurugenzi huyo ni kuangalia namna ya kuzungumza na wafanyakazi wake na kufahamu changamoto zinazowakabili kabla ya kuanza kufunga geti.

“Hili ni jiji kuna changamoto nyingi, baadhi ya wafanyakazi wanaishi Usagara na Buhongwa na asubuhi wanapokuja kazini kuna msongamano wa gari barabarani,” amesema Waryama.

error: Content is protected !!