MTENDAJI wa tarafa ya Ruaha, wilayani Ulanga, mkoani Morogoro, George Kayora, ameieleza mahakama jinsi baadhi ya viongozi wa ngazi ya kitongoji wilayani Ulanga, walivyoshirikiana na wananchi kula njama za kutaka kumuua. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)
Kayora alieleza hayo juzi wakati akitoa ushahidi wake kwenye kesi ya shambulio la kuhudhuru mwili lililotokea Juni 17 2022, katika kitongoji cha Kitope, wilayani Ulanga, mkoani Morogoro.
Kayora ambaye ndiye shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alidai mbele ya Mahakama ya wilaya ya Ulanga kwamba waliohusika kula njama za kutaka kumuua ni baadhi ya viongozi wa ngazi ya kitongoji.
Akiongozwa na Mwendesha Mashitka wa Jamhuri, Inspekta Rajabu, Kayora aliwataja viongozi aliodai wamekula njama kutaka kumuua kuwa ni Osward, (Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitope, kijiji cha Mzelezi) na Charles Madonda (Katibu wa CCM, kata ya Chirombola).
Aliendelea kudai kuwa viongozi hao ambao wote ni washitakiwa katika kesi hiyo, walishirikiana na mchimba madini aliyemtaja kwa jina la Dendelege, kufanya shambulio hilo ambalo nusura auawe.
Aliendelea kueleza kuwa viongozi hao waliwakusanya wananchi na kutoa maagizo ya kumshambulia mtendaji huyo wakati akitekeleza majukumu yake.
Alidai alikwenda katika eneo la kijiji cha Kitope kusimamia utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngolo Malenya aliyeagiza kutoruhusu shughuli za uchimbaji madini unaofanywa kiholela katika eneo hilo ambalo ni hifadhi ya barabara.
“Mheshimiwa hakimu, viongozi hawa ndio waliokula njama kwa kushirikiana na wananchi ili wanishambulie kwa lengo la kutaka kuniua, alidai Kayora.
Alieleza kuwa siku ya tukio wakati akienda kwenye eneo la machimbo ya madini ya rubi, kwa namna ya kustaajabisha Osward alimsimamisha barabarani akiwa na kundi la wananchi, kisha Madonda aliwaamuru wananchi kumshambulia.
“Wakati wananchi wananishambulia, viongozi hao waliungana na wananchi, wakaendelea kutoa maelekezo ya kuhamasisha wanipige.
“Nilipigwa kwa mawe, magongo na kukatwa na kitu chenye ncha kali mkono wangu wa kushoto na kusababisha kuvuja damu nyingi sana,” alidai Kayora
Pia alidai katika shambulio hilo, aliteguka bega lake la kulia na kupata maumivu makali yaliyopelekea apate rufaa katika Hospital ya Mtakatifu Francis ya Ifakara, akitokea hospitali wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro.
Alieleza mahakama kuwa ana mshukuru mkuu wa wilaya ya Ulanga, Ngolo Malenya na viongozi wote wa wilaya chini ya Mkurugenzi Mtendaji kwani walipambana kuokoa maisha yake na kufanikiwa kuwanasa wahusika ambao wapo hapo mahakamani.
Tukio la kushambuliwa kwa mtendaji huyo, pia lililaaniwa vikali na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali Za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa na kuagiza wahusika wafikishwe kwenye mikono ya sharia.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa tena Agosti 18 mwaka huu mahakamani hapo.
Leave a comment