June 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mtatiro mwenyekiti CUF

Spread the love

JULIUS Mtatiro, mwanasiasa machachari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii nchini,  ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya uongozi ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), anaandika Jabir Idrissa.

Mtatiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, ataongoza kamati inayojumuisha Ahmed Katani na Severina Mwijage ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT).

Katani ni Mbunge wa jimbo la Tandahimba, mkoani Mtwara wakati Severina alikuwa mjumbe wa kamati kama hiyo ilipoteuliwa Agosti mwaka jana mara baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu uenyekiti kwa barua ya 5 Agosti.

Uteuzi huo uliotangazwa leo na Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar,  umefanywa na Baraza Kuu lililofanya kikao cha siku moja jana mjini Zanzibar.

Kikao cha baraza kuu ambacho kikatiba, kimekasimiwa madaraka ya Mkutano Mkuu wa Taifa, kimefanyika katika hatua ya kukabiliana na hali ya hewa iliyochafuka baada ya kundi la wanachama “walioasi” kuvamia mkutano mkuu maalum uliofanyika 21 Agosti jijini Dar es Salaam ukiwa na agenda ya kuchagua mwenyekiti mpya.

Mkutano huo pia ulikuwa utumike kumchagua makamu mwenyekiti kutokana na Juma Duni Haji naye kujiuzulu Agosti mwaka jana, yeye akiwa ameidhinishwa na chama ili kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa rais Oktoba mwaka jana.

“Kwa kuzingatia kwamba kutokamilika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa, kulisababisha kushindwa kufanyika kwa uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chama, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limetumia uwezo liliopewa na Katiba ya Chama, Ibara ya 101 na 118, kuunda Kamati ya Uongozi ambayo itakuwa ikifanya kazi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti hadi hapo uchaguzi wa kujaza nafasi hizo utakapofanyika,” imesema taarifa ya Mazrui.

Baraza pia limemteua Joram Bashange kukaimu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbarala Maharagande kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma hadi hapo nafasi hizo zitakapojazwa rasmi kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Chama hicho.

Bashange ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Fedha wa chama, anashika kwa muda nafasi aliyokuwepo Magdalena Sakaya, Mbunge wa Kaliua, mkoani Tabora ambaye ni mmoja wa viongozi 11 wa juu akiwemo Prof. Lipumba, ambao uanachama wao umesimamishwa na Baraza Kuu hilo.

Naye Maharagande anachukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Abdul Kambaya ambaye yumo katika orodha ya viongozi waliosimamishwa uanachama kufuatia tuhuma za kuongoza vurugu zilizosababisha kuvunjika kwa mkutano mkuu maalum.

Viongozi wengine waliosimamishwa mpaka watakapofika kujielezambele ya Baraza Kuu, ni Ashura Mustapha, Omar Mhina, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.

Ashura ni mjumbe wa Baraza Kuu na mwanamama aliyewahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma CUF wakati Mnyaa na Kombo, walikuwa wabunge kipindi cha 2010/2015; Mnyaa akiwakilisha jimbo la Mkanyageni na Kombo jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.

Taarifa ya Mazrui imesema hatua ya kuadhibu viongozi hao imetokana na kuthibitika kuwa waliongoza vurugu ambazo chama kinaamini zilipangwa makusudi kwa nia ya kukihujumu.

Viongozi hao wametajwa kuwa walishirikiana na maadui wa chama walio ndani na nje na kwamba walikaidi hata walipotakiwa kurekebisha mwenendo wao “huo mbaya dhidi ya chama.”

 

error: Content is protected !!