Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ‘Mtatiro amefuata fursa kwa JPM’
Habari za Siasa

‘Mtatiro amefuata fursa kwa JPM’

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa chama cha CUF, Julias Mtatiro akizungumza na waandishi wa habari
Spread the love

KWENYE siasa hatufuati watu. Ukiwafuata watakuacha solemba. Fuata misingi. Anaandika Ansbart Ngurumo … (endelea).

Msando na Mtatiro walikuwa wafuasi. Hawakuwa waanzilishi. Hata wangekuwa waanzilishi, tungewaacha waende zao kama tulivyowaacha akina Prince Bagenda na Chifu Abdallah Fundikira; au hata mgombea ubunge wa kwanza wa Chadema, Dk Amani Kabourou.

Msando na Mtatiro hawafikii hata nusu ya Dk. Slaa. Hawa ni vijana wanaotafuta fursa.

Tambua pia sababu ya adui kutumia dola kuminya wapinzani. Anajua wapo wepesi watakaoumia na kuachia haraka, na kumwomba awakumbuke katika ufalme wake.

Anajua kuna wafuasi wao watakaokufa moyo kwa sababu ya imani waliyokuwa nayo kwa hao wanaoondoka.

Anajua kuwa hatua hiyo itagusa wengine, nao wakate tamaa ya kuunga mkono mapambano.

Asichojua ni kwamba hatafaulu kuchukua au kushinda mioyo ya wote. Asichojua ni kwamba anatengeneza upinzani mkali ndani ya mfumo wake, ambao utatumika kuangusha mfumo huo.

Asichojua ni kwamba kuna watu wavumilivu na wastahimilivu wasiotikiswa na mbwembwe hizi.

Asichojua yeye na hao wanaoondoka ni kwamba kama angefanikiwa kuua upinzani ndiyo yangekuwa maangamizi makubwa ya taifa.

Katika mazingira kama haya, tupo wengine tunaoamini kwamba upinzani hauwezi kufa bali utakuwa imara zaidi kwa sababu kiwango kile kile cha nguvu inayotumika kuuangusha ndicho kitakachotumika kuusimika.

Sisi wengine ni watu wa misingi, si wafuasi wa watu. Kama ni mtu, tutakuwa nawe iwapo tu unatetea misingi ile ile iliyotukutanisha.

Ukiachana na misingi yetu hatukung’ang’anii wala hatukulili, maana wewe pia hutulilii.

Nimesikiliza hotuba ya Mtatiro mbele ya waandishi wa habari. Kijumla, yale yalikuwa *maombi ya kazi* kwa JPM.

Ndiyo maana amesisitiza kuwa ametafakari na kufanya personal analysis. Haya mambo hayashuki ghafla kutoka popote yatokako.

Mtatiro anaona amechelewa. Kuna vijana anaowaonea wivu ambao JPM amewaona na kuwapa fursa mapema. Hataki kuachwa nje.

Rais yule yule, ambaye Mtatiro majuzi tu aliandika mitandaoni akihoji, “rais ni kitu gani?” ndiye huyo ambaye leo Mtatiro anasema anaenda kubwa balozi wake kutangaza sifa na kutetea mafanikio yake.

Kwa Mtatiro, serikali ikifanya jambo zuri, uamuzi sahihi ni kuacha chama chako ukajiunge nayo! Kwa Mtatiro, JPM hahitaji upinzani tena. Kwa Mtatiro, kukosoa serikali na kutaka irudi mstarini si kutumikia taifa.

Ni kweli, Mtatiro ameishiwa pumzi mapema; na nimeshamweleza hilo. Lakini wapo wengi walio na pumzi fresh kabisa. Shikamana na hao.

Mtatiro anatafuta fursa ambayo kwa mtazamo wake, haipo tena kwenye upinzani.

Kumbuka , alipotaka ubunge wa Ubungo, akagombea kupitia CUF, alijikwaa kwenye kisiki John Mnyika wa Chadema.

Alipoutaka tena kupitia Segerea, akajikwaa kwenye kigingi Anatropia Theonest wa Chadema.

Kwa hali ya siasa za CUF ambacho anaona kinakufa Bara, haoni tena pa kugombea.

Hata kwa kupitia Chadema, iwapo angejiunga nacho, haoni njia rahisi kwani majimbo yamejaa wagombea na watia nia watarajiwa; na anapotazama mikiki ya siasa hizi za kipolisi anapoteza tumaini kabisa.

Amedanganyika kwa ushindi wa akina Mtulia, Mollel na madiwani wengi tu waliojiondoa upinzani wakateuliwa kwenye upinzani, na wakashinda kwa lazima. Anaona njia nyeupe ipo kule.

Amedanganyika kwa akina David Kafulila, Moses Machali, Juliana Shonza, Patrobas Katambi na vijana wengine waliopata vyeo serikalini wakitokea upinzani.

Kifupi ni kwamba Mtatiro ameishiwa subira na amenaswa katika ulimbo wa JPM. Nawe umenaswa kirahisi?

Nimemsikiliza, nimemtazama usoni. Amechoka. Anataka pumziko. Kuna kitu anakimisi. Anakifuata kule.

Muache achoke peke yake. Kama nawe umechoka naye, pumzika. Sisi tunaendelea.

Kama ulifuata mtu, unaruhusiwa kundoka naye na kuzurura naye popote atakapokuwa. Kama upo nasi kwa sababu ya misingi, utabaki tu hata wakiondoka wote.

Kukata tamaa si chaguo bora, bali kubadili mbinu kulingana na hatua ya mapambano.

Nduguyo,
Ansbert Ngurumo

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Tanesco yawasha mtambo namba 8 Bwawa Julius Nyerere

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

error: Content is protected !!