May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mtanzania aula BOA

Spread the love

 

BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya Afrika Tanzania (BOA), imemteua Adam Mihayo kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa benk hiyo. Anaripoti Helena Mkonyi, TUDARCo … (endelea).

Taarifa ya Bodi hiyo kumtangaza Mihayo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Nyamajeje Wegorro ambapo awali Mkurugenzi alikuwa Joseph Iha Wanje, ambaye muda wake ulimalizika Aprili 2020.

“Zaidi ya uzoefu wa miaka 13 katika tasnia ya benki za ndani, kikanda na za kimataifa pia ana historia ya kukuza biashara za rejareja, SME na mashirika. Pia yeye ni mtaalam katika usimamizi wa majanga,” amesema.

Dk. Wegorro amesema kabla ya Mihayo kujiunga na benki hiyo alikuwa Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya Absa Tanzania Limited, ambapo alifanikiwa kuongoza kazi ya mikopo ya benki hiyo na kushiriki kikamilifu kufafanua malengo ya kimkakati kusaidia ukuaji wa biashara.

Amesema pia Mihayo aliwahi kuwa Mkuu wa Mikopo kwa Benki ya Stanbic Tanzania Limited.

“Adam alianza kazi yake ya kibenki katika Benki ya Kitaifa ya Biashara (NBC) ambapo alikuwa miongoni mwa wataalam wachache wa benki wenye talanta waliotambuliwa kwa Mafunzo ya Usimamizi katika Benki ya Absa nchini Afrika Kusini mnamo 2008.

Pia, ana Shahada ya Kwanza ya Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na amehudhuria kozi kadhaa za Uongozi na Usimamizi. Analeta benki seti ya kipekee ya ujuzi, na uzoefu ambao utasaidia sana kuipeleka BOA katika mafanikio mapya,” amesema.

Mwenyekiti huyo alisema ana imani kuwa uongozi wake katika kusimamia fedha na kibenki utaiwezesha benki kudumisha ushindani wake kwani inaendelea kuboresha huduma zake na utoaji wa bidhaa kwa wateja ambayo inaambatana na sera ya serikali ya kufanikisha maendeleo ya uchumi na mwingiliano wa kifedha nchini.

“Kwa niaba ya Bodi, ninamtakia Adam kila mafanikio katika kuongoza benki hiyo kufikia malengo yake kwa wadau wote,” alisisitiza.

error: Content is protected !!