April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mtangazaji maarufu afa kwa corona

Spread the love

ZORORO Makamba (30), mtangazaji maarufu wa vipindi vya televisheni nchini Zimbabwe, amefariki dunia kwa ugonjwa wa corona (COVID-19). Inaripoti mitandao ya kimataifa…(endelea).

Makamba aliyefariki jana tarehe 23 Machi 2020, amekuwa mtu wa kwanza kufariki kwa corona nchini humo, ambapo alikuwa miongoni mwa wawili wa kwanza waliopimwa na kubainika kuwashambuliwa na virusi hivyo.

Alipelekwa katika Hospitali Kuu ya Harare, baada ya kuzidiwa na mafua huku dalili mbalimbali za ugonjwa huo zikiendelea kudhihiri.

Imeelezwa, Makamba alipata virusi hivyo alipokuwa New York nchini Marekani. Baada ya kufika Zimbabwe na kufanyiwa vipimo, alitengwa na kuwekwa katika jengo pekee la Wilkins lililopo katika hospitali hiyo ya Harare, lililowekwa maalumu kwa wanaobainika kuwa na virusi hivyo.

Rafiki wa karibu wa Makamba akizungumza na kituo cha habari cha CNN amesema, rafiki yake baada ya kurejea alikuwa akisumbuliwa na mafua makali, homa za mara kwa mara pamoja na mwili kuchoka.

Monica Mutsvangwa, Waziri wa Habari wa Zimbabwe amesema amepokea taarifa za kifo cha Makamba kwa masikitiko “nimeshtushwa sana na kifo hicho.”

Taarifa iliyotolewa na Obadiah Moyo, Waziri wa Afya wa Zimbambwe imeeleza, Makamba alisafiri kwenda New York tarehe 29 February 2020 na kurejea Harare, Zimbabwe tarehe 9 Machi 2020. Alianza kuona mabadiliko ya afya yake siku chache baada ya kurejea.

Emmerson Mnangagwa, Rais wa Zimbabwe tayari ametangaza kufunga mipaka yote ya nchi hiyo isipokuwa kwa raia wa nchi hiyo wanaorejea nyumbani na magari ya mizigo.

Pia amepiga marufuku mikusanyo ya watu zaidi ya 50 na kufunga baa, klabu za usiku, majumba ya mazoezi (gyms) na maeneo ya kuogelea kutokana na tishio la corona.

error: Content is protected !!