August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mtandao wa wanafunzi wampinga Rais Magufuli

Rayson Elijah, Mwanasheria wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP)

Spread the love

KAULI ya Rais John Magufuli kuwataka wanafunzi wote wa kike wa shule za msingi na sekondari watakaopata ujauzito kutorejea mashuleni imeendelea kupingwa na makundi mbalimbali katika jamii, anaandika Irene David

Mbali na asasi takribani 25 za kiraia kupinga kauli hiyo, Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) nao wameomenyesha kuguswa na kauli hiyo.

Siti Ngwali, Mhazini wa mtandao huo, amesema kauli ya rais imekiuka katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba mingine ya kimataifa ambayo inatoa uhuru wa kupata elimu bila vizuizi vya namna yoyote watoto.

Mhazini huyo akizungumza na MwanaHALISI Online amesema maamuzi ya rais yanapelekea kusitisha ndoto za wanafunzi na hatua hiyo haiwezi kuwa suluhisho la kudumu la tatizo hilo.

Siti amemtaka rais kutengua kauli hiyo kwani inakiuka haki za binadamu ikiwemo haki ya kupata elimu na kutafuta njia mbadala ikiwemo kuwepo kwa mijadala itakayohusisha wadau wa elimu ndani na nje ya nchi ili kupata suluhisho la tatizo hilo.

Pia amemshauri mamlaka zinazohusika kutoa elimu ya jinsia na athari za mimba za utotoni ziendelee kutolewa ili kuendelea kuwasisitiza  wanafunzi dhidi ya athari za mimba za utotoni.

Kwa upande wake, Rayson Elijah, Mwanasheria wa taasisi hiyo, amesema kauli hiyo ya rais wameichukulia kama pigo lingine dhidi ya haki za wanawake na watoto wa kike.

Amesema serikali ni bora ijikite kuwashughulikia watuhumiwa wanaowapa mimba kuliko kuwashughulikia hawa watoto ambao wengi wao wapo chini ya umri wa miaka kumi na nane (18).

Elijah amesema anaamini rais ni msikivu na kwamba wanamuomba aliangalie swala hili kwa jicho la tofauti kama ilivyo kuwa katika suala la mchanga na madini.

error: Content is protected !!