Friday , 19 April 2024
Home Kitengo Maisha Afya Mtambo achangia ujenzi zahanati kijiji Dondo, wananchi…
AfyaHabari Mchanganyiko

Mtambo achangia ujenzi zahanati kijiji Dondo, wananchi…

Spread the love

 

MHANDISI Mohamed Mtambo, aliyekuwa mgombea Ubunge wa Mkuranga (ACT-Wazalendo) mkoani Pwani ametoa Sh.500,000 kuchangia ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Dondo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mhandishi Mtambo alitoa msaada huo mwishoni mwa wiki baada ya kuombwa na wananchi wa Kijiji cha Dondo, Kata ya Dondo Tarafa ya Kisiju Wilaya ya Mkuranga akiwa kwenye ziara ya kushukuru wananchi kwa kumpigia kura katika uchaguzi mkuu uliopita 2020.

Alisema suala la kuchangia, kuhamasisha maendeleo lisihusishwe na itikadi zozote za kisiasa kwa sababu changamoto za wananchi hususan suala la matibabu halichagui nani ataugua na wakati gani.

“Nimekuja hapa kuwashukuru kwa kunipigia kura mwaka jana 2020, nimeona si haki kuwakimbia kwa kuwa hatukushinda, nialikeni kwa shughuli zozote za kijamii zikiwemo hitima, harusi, hata kuchimba mitaro ya ujenzi wa zahanati yetu nitakuja.”

“Uzalendo kama lilivyo jina la chama chetu ni pamoja na kurudi kutoa shukrani, kuishi na watu kidugu, kuwaunganisha na si kuwagawa” alisema Mhandisi Mtambo.

Awali, akitoa kero ya changamoto ya ukosefu wa huduma za afya kijijini hapo, Maganga Lugutu alisema licha ya wananchi kujua umuhimu wa kuwa na zahanati, hali ngumu ya uchumi waliyo nayo inawakwamisha kufikia lengo hilo.

“Changamoto kubwa tuliyonayo kwa sasa ni kukosa huduma ya matibabu, mtu akiugua ni kazi kubwa kuweza kufika hospitali, kwa mfano umbali wa kutoka hapa Dondo hadi hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa usafiri wa pikipiki ni Sh.10,000 kwenda tu.”

“Bado dawa, vipimo na mgonjwa akilazwa shida inakuwa kubwa zaidi tunaomba serikali ituangalie kwa jicho la pekee kutuongezea nguvu kwani tunateseka sana kwa kukosa zahanati,” alisema Lugutu.

Akipokea sehemu ya mchango huo kwa niaba ya kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Dondo, Kata ya Dondo, Omary Seif Matope, alisema kata hiyo haijawahi kuwa na zahanati tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.

Alisema licha ya kata hiyo kuwa na idadi kubwa ya watu, shule moja ya msingi na sekondari wamekuwa wakifuata matibabu kwenye kata zingine ambazo zipo umbali mrefu na kijiji chao.

Matope alishukuru mchango huo wa fedha uliotolewa na Mhandisi Mtambo akisema utawasaidia kwenye ujenzi huo wa zahati.

“Hadi sasa wananchi kwa nguvu zetu tumeweza kufyatua tofari 2,800 huku mahitaji yakiwa ni tofari 10,500 hadi kukamilisha boma lote, kwa niaba ya wananchi wa Dondo namshukuru huyu kijana wetu kwa kutushika mkono, ni rai yangu niombe wengine mfano huu wa kujitoa kwa ajili ya wengine,” alisema

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari Mchanganyiko

Mume auwa mke kwa kumchoma visu, ajisalimisha Polisi

Spread the loveJACKSON Kalamji (49), anashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza,...

error: Content is protected !!