January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mtaala wa urekebishaji wahalifu wakamilika

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Sifuni Mchome (katikati) akifungua kikao cha wadau kujadili mitaala ya mafunzo ya urekebishaji wafungwa. Wa pili kushoto ni Kamishina wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Juma Malewa. Kikao hicho kimefanyika katika hoteli ya Protea Courtyard, jijini Dar es Salaam.

Spread the love

JESHI la Magereza nchini, limetakiwa kuzingatia mawazo yatakayotolewa na wadau katika kukamilisha maandalizi ya mitaala ya mafunzo ya urekebishaji wa wahalifu. Anaandika Pendo Omary…(endelea).

Rai hiyo imetolewa na Prof. Sifuni Mchome – Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau kujadili mitaala ya mafunzo ya urekebishaji wafungwa.

Kikao hicho kimefanyika leo katika hoteli ya Protea Courtyard jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na tasisi za kijeshi na elimu.

Prof. Mchome amesema, “nawasihi kuzingatia ipasavyo mawazo yatakayotolewa na wadau hawa katika kukamilisha maandalizi ya mitaala ya mafunzo ya urekebishaji.”

“Kukamilika kwa mitaala hiyo yenye maoni ya wadau siyo tu kutawasaidia kupata usajili kwenye Baraza la Taifa la Elimu na Ufundi (NACTE) bali kutawezesha pia kutoa mafunzo stahiki ya taaluma ya urekebishaji na hivyo kuliwezesha Jeshi la Magereza kutekeleza kwa ufanisi jukumu la urekebishaji wa wahalifu,”amesema Mchome.

Pia, amesema wafungwa wanapomaliza vifungo vyao na kurudi kwenye jamii wakiwa wamerekebika na kupata ujuzi itasaidia kuwawezesha kuendesha maisha yao wakiwa raia wema.

Kupatikana kwa mitaala iliyosajiliwa na Baraza la Taifa la Ithibati kutawezesha mafunzo ya taaluma ya urekebishaji kutambulika kitaifa na kimataifa, hali itakayochangia kulitangaza Jeshi na nchi ndani na nje ya bara la Afrika.

“Chukueni hatua katika maandalizi ya mambo ya msingi yatakayosaidia utekelezaji wake. Mambo hayo ni pamoja na miundombinu ya vyuo vitakavyotoa elimu kwa kutumia mitaala husika, vifaa vya kufundishia, walimu wenye viwango vya elimu inayokubalika na kufanya mapitio ya mitaala,” ameongeza Mchome.

Akizungumza kwa niaba ya John Minja- Kamishna Jenerali wa Magereza, Juma Malewa- aliye Kamishina wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, amesema hatua hiyo ni sehemu ya kufanya maboresho katika maeneo kadhaa ili kulifanya jeshi hilo liendane na wakati na kutekeleza majukumu yake kisayansi na kwa ufanisi unaotarajiwa.

“Kukamilika kwa mitaala ya mafunzo ya urekebishaji kutawezesha kuboresha utendaji kazi kwa maafisa na askari, hali itakayosaidia Jeshi la Magereza kutekeleza wajibu wake ipasavyo,” amesema Malewa.

Aidha, Malewa amesema wanafunzi kutoka mataifa mengine wataweza kuja kupata mafunzo hayo hapa nchini kwa kuwa yatakuwa yanatambulika kimataifa.

error: Content is protected !!