August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msuya: Mjadala wa Katiba uishe

MZEE MSUYA ATAKA MJADALA WA KATIBA UISHE/ATOA MAONI KWENYE KIKOSI KAZI
Spread the love

WAZIRI Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya amesema ingependeza iwapo mchakato wa Katiba mpya ungefikia mwisho, ili kuruhusu Watanzania kufanya kazi, huku akisisitiza elimu ya urai kwa wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Msuya aliyasema hayo leo tarehe 19 Julai, 2022 baada ya kuwasilisha maoni yake mbele ya Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan cha kuratibu  maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

Ushauri wa Mzee Msuya kuhusu Katiba mpya ni mwendelezo wa viongozi waandamizi ambao wamepata nafasi ya kutoa maoni mbele ya Kikosi Kazi cha Rais Samia akiwemo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mstaafu Jaji Damian Lubuva, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mstaafu Profesa Mussa Assad.

Pia hitaji la Katiba mpya limezungumziwa na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) na wengine.

Waziri Mkuu huyo mstaafu amesema ni vizuri suala la  Katiba kufikia mwisho,  huku akishauri iwapo kuna taarifa mpya za kuongezwa mchakato ufanyike ili Katiba ipatikane.

Amesema haipendezi kila mwaka Watanzania kurudia kudai Katiba kila mara na kwamba watu wanatakiwa kufanya kazi kujenga nchi yao.

“Serikali ifikirie namna ya kufunga mjadala wa kupatikana Katiba mpya, ili watu walijenge Taifa lao badala ya kuendelea kusikia mijadala ya  Katiba kiloa kukicha,” amesema.

Kuhusu ni kitu gani kitambulie kati ya Tume Huru ya uchaguzi na Katiba Mpya, Waziri Mkuu Msuya alisema suala la kujua sehemu ya kuanzia waachiwe viongozi wa Serikali, huku akisisitiza kuwa mjadala wa Katiba unatakiwa kufikia mwisho.

Msuya amesema Rais Samia ameanza kazi vizuri, hivyo ni jukumula la kila Mtanzania kumuunga mkono ili kuchochea mafanikio ambayo yameanza kuonekana.

“Haya mambo ya kupanga kipi kitangulie waachiwe viongozi wetu wa kiserikali ndio wanaojua mambo zaidi lakini nataka mjadala wa Katiba mpya umalizike upesi iwezekanavyo kwa uratibu ambao watajipanga wao,” amesema Msuya.

error: Content is protected !!