October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msukuma ‘akabidhi’ ubunge wake kwa JPM 

Spread the love

JOSEPH Kasheku (Msukuma), Mbunge wa Geita (CCM), ameweka rehani ubunge wake kwa Rais John Magufuli kwa ahadi kwamba, iwapo uchunguzi utafanywa na kubaini kuwa, taarifa ya madini ya dhahabu yanayochimba Geita ni sawa na taarifa zilizopo wizarani, basi atajiuzulu. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Mbunge huyo amemwomba Rais John Magufuli kuagiza jeshi kwenda mkoani Geita, kuchunguza kiasi cha madini ya dhahabu yanayochimbwa mkoani humo na taarifa halisi zinazofikishwa wizarani.

Mbele ya Rais Magufuli, akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 7 Juni 2019, Msukuma amesema kuwa, serikali hupewa taarifa za uongo kuhusu kiasi cha madini yanayochimbwa mkoani humo na kwamba, kama kukifanyika uchunguzi na kubainisha kwamba, madai yake ni uongo, atajiuzulu ubunge.

Amesema, pengine changamoto hiyo inatokana na udhaifu wa wasimamizi wa serikali, hivyo kwa kuwa, jeshi linaaminika kwa uadilifu, ameshauri kipelekwe kikosi komoja cha jeshi kwa muda ili kufuatilia mwenendo wa uchimbaji madini hasa ya dhahabu mkoani Geita.

“Sasa najiuliza, pengine kuna udhaifu kwa wale wasimamizi…, kama unaweza kutoa kikosi kidogo cha jeshi, kikakae Geita, kizunguke ukikosa tani moja au mbili kwa siku. tena wakivaa unifomu , mimi niko tayari kujiuzulu ubunge,” amesema Msukuma.

Mfanyabiashara huyo wa madini ameeleza kuwa, idadi ya dhahabu kiasi cha kiligramu 600 kilichoandikwa katika bajeti ya madini,  kwamba yamechimbwa mkoani Geita katika kipindi cha mwezi Januari hadi Mei 2019, ni uongo.

Msukuma amesema, udanganyifu huo amekuwa akiueleza bungeni mara kadhaa lakini mawaziri hawakumsikiliza, na kwamba, ameamua kumfikishia taarifa hizo Rais Magufuli akiamini kwamba, ataifanyia kazi.

“Nilikuwa naangalia rekodi ya mkoa wangu wa Geita ambao ni kinara wa dhahabu toka mwezi wa kwanza mpaka wa tano. Tunaenda kusoma bajeti ya madini tumekusanya dhahabu kg 600.

“Nilizungumza bungeni lakini pengine mawaziri huwa hatusikilizwi vizuri.  Lakini nikaona bora wewe nikueleze, hata theluthi ya dhahabu hatujaweza kuikusanya, kwa siku moja tunaweza kukusanya tani moja,” amesema Msukuma.