July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Msongola, Chanika kinara migogoro ya ardhi

Spread the love

MSONGOLA, Chanika katika Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam yanaongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi, anaandika Regina Mkonde.

Migogoro hio imesababishwa na baadhi ya wenyeviti wa vijiji na serikali za mitaa wasio waaminifu.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Paul John Mbembela, Ofisa Mipango Miji na Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilala amesema kuwa, usimamizi mbovu katika uuzwaji wa viwanja unaofanywa na baadhi ya wenyeviti ndiyo sababu ya migogoro ya ardhi.

Amesema kwamba, mara kwa mara kiwanja kimoja kimekuwa kikiuzwa kwa watu wawili tofauti na kwa wakati tofauti.

“Baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa ndiyo chanzo cha migogoro ya ardhi katika maeneo ya pembezoni mwa wilaya ambayo wananchi wengi wanakimbilia kununua viwanja, hususan kwenye maeneo ambayo huduma ya upimwaji viwanja haujafika,” amesema na kuongeza;

“Hali kadhalika hivi karibuni zimetokea kampuni nyingi zisizosajiliwa ambazo zinajihusisha na uuzaji wa viwanja kwa wananchi, baadhi ziko kihalali na zimesajiliwa.”

Ametaja maeneo yaliyokithiri migogoro hiyo, ikiwemo maeneo ya Chanika mwisho, Kimwani na Msongola.

“Wananchi inabidi wawe makini, waache kukurupa katika ununuzi wa ardhi kwa kuwa, hivi sasa maeneo ya mijini kumejaa na kwamba wanakimbilia pembezoni mwa miji.

“Mfano katika wilaya yetu, ardhi ya Chanika hivi sasa inanunuliwa na watu wengi, nashauri kabla ya mtu kununua ardhi hususan iliyomo katika Manispaa ya Ilala, aulize kwanza katika serikali za mitaa husika na ikiwezekana hata katika ofisi zetu ili kujiridhisha kama eneo hilo halina utata,” amesema.

Pia amewataka wenyeviti wa mitaa kuwa makini pindi wanapohusika katika uuzaji wa viwanja kwa kuangalia matumizi ya ramani ili kujua matumizi sahihi ya ardhi anayonunua.

error: Content is protected !!