October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msimamo wa JPM wamtisha RC Mbeya

Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya

Spread the love

ALBERT Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC) alikuwa na mpango wa kwenda kugombea ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini, lakini amefuta wazo hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).

Akizungumza leo Jumanne tarehe 7 Julai 2020 jijini Mbeya amesema, hatokwenda tena kugombea jimbo hilo kwa kuwa, hawezi kwenda kinyume na kauli ya Rais wa Tanzania John Magufuli aliyoitoa jana Jumatatu, kuwa ‘anayetaka ruksa ya kugombea, aandike barua lakini nafasi yake itajazwa.’

Wakati akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, Ikulu Chamwino, jijini Dodoma Rais Magufuli alisema, “ili kazi ziendelee, taifa hili lazima liendelee na matatizo ya wananchi lazima yatatuliwe kila siku.”

“Hayawezi kusubiri mtu ameomba ruksa mpaka ukarudi huko ruksa ikishindikana, haiwezekani.  Huo ndio ukweli.” alisema.

            Soma zaidi:-

Kutokana na kauli hiyo ya Rais Magufuli, RC Chalamila amesema, atabaki kwenye nafasi hiyo ya ukuu wa mkoa ili aendelee kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani humo.

“Nilikuwa miongoni mwa watia nia ya kugombea ubunge Iringa mjini, kwa sasa sintofanya hivyo zaidi ya kuendelea kuwatumikia wananchi wa Mbeya na kutii maelekezo ya Rais Magufuli,” amesema Chalamila.

Mchungaji Peter Msigwa, ndiye mbunge anayemaliza muda wake kwenye jimbo hilo.

Kwa sasa ametangaza nia ya kugombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akizungumza na MwanaHALISI Online hivi karibuni, Mchungaji Msigwa alisema endapo hatopata ridhaa ya kugombea urais kupitia chama hicho, atarejea Iringa Mjini kupambana ili kuendelea kuongoza jimbo hilo.

error: Content is protected !!