July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Msimamo Ukuta, DC apagawa

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa

Spread the love

HOFU ya wateule wa Rais John Magufuli sasa inashika hatamu. Wanahaha kuyumbisha dhamira ya mikutano na maandamano ya Septemba Mosi, anaandika Dany Tibason.

Mikutano na maandamano hayo yamesisitizwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta nchini (Ukuta).

Msimamo wa kufanya maandaman na mikutano hiyo ulitangazwa na Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Julai mwaka huu.

Christana Mdeme, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma amewaomba viongozi wa dini mkoani humo wawazuie waumini wao kushiriki kwenye maandamano na mikutano ya Ukuta.

Kauli hiyo imetolewa leo wakati Mdeme alipokutana na Viongozi wa Dini wa Mkoa wa Dodoma ambao unaunda Baraza la Amani la Mkoa.

Amedai, maandamano na mikutano ambayo inalenga kufanywa na Chadema ni haramu kwamba, watakaoshiriki watakuwa wamevunja Katiba ya Nchi na kwamba, watakanatwa.

Mbali na hilo amepiga marufuku kuvaa fulana zenye maneno (Ukuta) anayodai ya uchochezi au ambayo yana malengo ya kumdhalilisha rais wa nchi.

“Sasa nataka kuwaeleza viongozi wangu kwa taarifa zisizo rasmi, nasikia kuwa wameamua kuwatanguliza akina mama wajawazito katika maandamano hayo.

“Naomba akina baba msiwaruhusu akina mama kuwepo katika maandamano hayo kwani huwezi kujua mimba ya mama huyo mtoto atakayezaliwa ndiye Mkuu wa Wilaya, Askofu, Shekhe ama kiongozi mwingine wa ngazi ya juu,” amesema Mdeme na kuongeza;

“Kutokana na hali hiyo, nawaomba akina mama msikubali kutangulizwa katika maandamano hayo na mikutano maana mtaweza kuumizwa.”

Amesema, Septemba Mosi katika Mji wa Dodoma kutakuwa na ulinzi mkali ili kukabiliana na hali inayoweza kutokea.

Kuhusu madai ya Chadema kudai Katiba ya Nchi ambayo inaonekana kusiginwa kwa kuwanyima wapinzani kufanya siasa Mdeme amesema, pamoja na kuwepo kwa Katiba lakini yeye anasimamia sera ya ‘Hapa Kazi Tu.’

Alipoombwa kutoa ufafanuzi kama anaijua vyema Katiba na namna inavyozungumzia kuwepo kwa vyama vingi na utendaji kazi wa siasa amesema, ni kweli nchi inatakiwa kufanya kazi kwa misingi ya Katiba ya Nchi lakini “mimi anatekeleza sera ya ‘Hapa Kazi Tu.’

“Najua kuwa Katiba ya Nchi inataka kuwepo kwa demokrasia lakini kwa sasa hatuhitaji kufanya siasa bali tunatakiwa kutekeleza sera ya Hapa Kazi Tu” ameeleza Mdeme.

Wakati huo viongozi wa dini wamesema kuwa, kazi kubwa waliyonayo ni kulinda amani.

Ashamed Saidi, Mwenyekiti wa Baraza la Amani la Viongozi wa Dini ambaye ni Kaimu Shekhe wa Mkoa amesem, kazi kubwa ya viongozi wa dini ni kulinda amani.

Amoni Kinyunyu, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma ameitaka serikali kukaa meza moja na viongozi wa serikali kuhakikisha wanamaliza mgogoro huo.

Wakati huo huo Mdeme amesema, Septemba Mosi wilaya itafanya mapokezi ya Kassimu Majaliwa, Waziri mkuu ambaye anahamia Dodoma rasmi.

Amesema, mapokezi hayo yatafanyika katika Kata ya Mtumba na Waziri Mkuu ataenda moja kwa moja katika uwanja wa mpira wa Jamhuri kwa ajili ya kujitambilisha kwa wananchi.

…………………………………………………………………………………………………..

Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia (bonyeza)> Simgazeti kwa wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel. Pia unaweza kupakua (download) app ya Mpaper au Simgazeti kutoka kwenye playstore.

error: Content is protected !!