July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msimamizi mifuko ya hifadhi asema hali nzuri

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania (SSRA), Irene Isaka

Spread the love

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania (SSRA), Irene Isaka amesema si kweli kwamba mifuko ya hifadhi ya jamii ina hali mbaya kifedha.

Ingawa amekiri kuwa yapo matatizo katika uendelevu wake, lakini serikali iko macho ili mifuko hiyo isifikie kuonekana ina hali mbaya kiasi cha kuwa hatarini kufilisika.

“Ni kweli kama serikali inadaiwa fedha nyingi na baadhi ya mifuko lakini kinachodaiwa ni fedha ahadi ya fedha si mikopo,” amesema.

“Siyo kwamba serikali imekopa kwenye mifuko hii fedha inazoelezwa kuwa inadaiwa. Hizi ni fedha ambazo serikali inawajibu wa kuzitoa kama mchango wa wafanyakazi wake.

“Tukizungumzia fedha ambazo serikali imetoa udhaini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambazo mikataba ya utoaji lazima iheshimiwe, mifuko inaendelea vizuri,” alisema.

Isaka ameeleza hayo mbele ya wahariri wa vyombo vya habari nchini waliokuwa katika ziara maalum ya kukagua miradi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF), eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, wahariri walijionea miradi mikubwa ya uwekezaji ya ujenzi wa daraja la Kigamboni lililo katika asilimia 60 ya kukamilika pamoja na mradi ya nyumba 3,400 za kisasa eneo la Dege, ambayo NSSF inaiendesha kwa ushirikiano na serikali na sekta binafsi.

Ilikuwa katika majadiliano ya miradi hiyo, ndipo hoja ya hali ya mifuko ya hifadhi ya jamii ilichukua sehemu kubwa ya mjadala, huku wahariri wakiporomosha maswali kwa mkuu wa SSRA, mamlaka iliyoanzishwa kwa ajili ya kusimamia uendeshaji wenye nidhamu wa mifuko hiyo.

Isaka alisema uamuzi wa kuanzisha mfumo mpya wa ukokotoaji mafao ya wastaafu katika mifuko hiyo ni moja ya hatua za kuwezesha mifuko hiyo kuwa na viwango vinavyofanana vya ukokotoaji vinavyonufaisha wananchi wanaotoa michango katika mifuko.

Alisema moja ya majukumu ya SSRA – Social Security Regulatory Authority –  ni kuhakikisha mifuko inakuwa endelevu, inayotoa mafao mazuri hapohapo kuhakikisha kwamba maslahi ya wafanyakazi katika haki zao yanalindwa kwa kuwa wao ndio wachangiaji wa mifuko.

“Haiwezekani sisi tuwe pale kuibeba serikali kila jambo. Pamoja na kuwa hata sisi ni taasisi ndani ya serikali, hata sheria ya kuwepo kwetu imelenga kusaidia mifuko kuendeshwa kwa ufanisi na wafanyakazi walindwe haki zao. Kwa jukumu hili tunakwenda vizuri na nyinyi vyombo vya habari mnatusaidia sana,” alisema.

Katika mada aliyotoa kwenye semina alisema NSSF ndio mfuko wenye hali nzuri na unaotoa mafao mazuri zaidi.

NSSF linaendesha mradi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni kutokea eneo la Kurasini kwa kujumuisha na barabara ya kilomita moja, kwa kushirikiana na serikali ambayo imedhamini asilimia 40. NSSF yenyewe inagharamia mradi kwa asilimia 60.

Gharama za mradi huo unaojengwa na kampuni ya ACE ya Misri kwa ahadi kuwa ukamilike Julai 2015, ni Dola 235 milioni.

Mradi wa nyumba 3,400 za kisasa unatekelezwa chini ya mpango wa ubia kati ya kampuni binafsi na NSSF.

Wahariri wamesifia miradi hiyo miwili kama uwekezaji wenye viwango vya kimataifa kwa kuwa urejeshaji wa fedha zilizotumika, umejengewa utaratibu unaoeleweka.

Nyumba zinazojengwa Dege, zitauzwa kwa wahitaji kwa utaratibu utakaoanza mwezi ujao. Kila moja itauzwa kwa kati ya Dola 90,000 na 240,000 na yeyote atakayehitaji, bila ya kujali ni Mtanzania au la, atauziwa akitimiza masharti.

error: Content is protected !!