December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msilalamike, tunadhibiti uhalifu – Mwinyi

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Spread the love

 

MALALAMIKO yaliyojaa mitaani yakihusu mfumo wa kukabiliana na kukua kwa kiwango cha uhalifu Zanzibar hayajamsukuma Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kubadilika. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Kumekuwa na lawama nyingi mitaani kipindi cha wiki za karibuni baada ya kuripotiwa majeruhi kadhaa kutibiwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini hapa wakijieleza kuwa wamepigwa na askari wa vikosi vya serikali baada ya kuvamiwa makwao.

Taarifa za zinasema hospitali hiyo ya serikali ambayo ndiyo kubwa kabisa ya rufaa hapa, imepokea majeruhi wapatao 25 na kutibiwa majeraha yaliyotokana na kupigwa kwa kukatwa vitu vyenye ncha kali na kugongwa maeneo yenye mifupa.

Kwa mujibu wa mashuhuda, majeraha hayo ni vipigo na mashambulizi yaliyofanywa nyakati za usiku na askari hao ambao desturi yao hujifunika nyuso na kuvaa mararu huku baadhi wakibeba bunduki bali wengi wao wakiwa na silaha za jadi zikiwemo mapanga, mashoka, mapande ya nondo na nyaya.

Gazeti hili limeelezwa kuwa askari wanojulikana kwa maarufu kwa jina la Mazombi, wameibuka upya na inaonekana “wameelekezwa” kuvamia makazi ya wananchi na kudhibiti vijana wanaoshukiwa kwa uhalifu wa kupora watu kwa mtindo wa kuwavizia wanapokuwa njiani kurudi makazini.

Gazeti limefanikiwa kuwadikia majeruhi sita waliojeruhiwa na kutekelezwa mbali na makwao walikokutwa na kuchukuliwa.

“Mie nilikuwa nimelala nikajikuta nimeamka kwa vishindo vya watu waluokuja nyumbani usiku wa manane na kulazimisha nitoke nje. Nilipokataa wakavunja mlango na kunitoa huku wakianza kunishambulia. Walinizungusha mitaa kwa mitaa hadi Mbuzini walikoniachia huku nikiwa sijiwezi na damu zikimwagika maeneo mbalimbali ya mwili. Hawakunieleza kosa langu na mie sijafanya uhalifu wowote,” alisema kijana aliyetaka asitajwe jina gazetini.

Taarifa zinasema mazombi walipita mitaani wakiwa na orodha ya watu wanaosemekana wametajwa na ofisi za masheha kuwa ni “vijana wakorofi mfano wa panyaroad” wale vijana wanaopora wananchi kwenye mitaa ya jiji la Dar es Salaam.

Hatua hii mpya inayolalamikiwa inakuja wiki moja tu tangu Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis alipohutubia mikutano na wananchi kwenye shehia za mjini Zanzibar kwa agenda ya kutaka ushirikiano ili.kudhibiti uhalifu unaokua kwa kasi.

Mikutano ya Kamishna Hamad ambaye aliahidi kuteua inspekta kwa kila shehia wa kuongoza ulinzi kupitia program ya Polisi Jamii, ilifuatiwa na taarifa za baadhi ya askari polisi kisihi ndugu zao kujiepusha na kukaa vijiweni usiku.

Askari wa vikosi vya SMZ “mazombi” ni maarufu kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza mitaani nyakati za uchaguzi mkuu. Operesheni zao huacha makumi ya watu wanaosadikiwa kuwa wapinzani wakiwa hoi kwa kuumizwa viungo.

Rais Dk. Mwinyi akizungumza na waandishi wa habari leo alisema wananchi wasiwe na hofu na kwamba uhalifu utakuwa historia muda si mrefu ujao.

“Ninafahamu suala hili na nimemwambia Kamishna wa Polisi sitaki kusikia kuna ongezeko la uhalifu hapa. Kamishna amenihakikishia utadhibitiwa kwa hivyo wananchi wasilalamike wanapoona hatua zinachukuliwa za kudumisha amani na kuleta utulivu.”

error: Content is protected !!