October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mshtakiwa alivyomaliza kujitetea kesi ya Mbowe, wenzake

Spread the love

 

ADAM Kasekwa, mshtakiwa wa pili katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, amemamliza kutoa utetezi wake kwenye shauri dogo la kesi hiyo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kasekwa amemamliza kutoa ushahidi wake leo Jumatatu, tarehe 27 Septemba 2021, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Mustapha Siyani, baada ya kuulizwa na kuhojiwa na mawakili wa utetezi pamoja na mawakili wa Jamhuri.

Kasekwa alianza kutoa ushahidi wake Ijumaa, tarehe 24 Septemba 2021, katika kesi hiyo ndogo ndani ya kesi kubwa iliyotokana na pingamizi la utetezi kupinga maelezo yake ya onyo yasitumike mahakamani hapo kama ushahidi, kwa madai yalichukuliwa kinyume cha sheria.

Tangu alipoanza kutoa ushahidi wake mahakamani hapo, Kasekwa amedai mchakato uliotumika kumkamata, kumuweka kizuizini na uandikishwaji wa maelezo yake ya onyo hayakufuata sheria.

Miongoni mwa mambo yaliyoibuka katika ushahidi wake, ni utambuzi wa watu aliodai walimkamata kwa nguvu, vituo vya polisi alivyowekwa mahabusu baada ya kukamatwa, mateso aliyoyapata akiwa kizuizini na vitu alivyodaiwa kubambikiziwa alipokamatwa tarehe 5 Agosti 2020 maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kasekwa alidai, baada ya kukamatwa aliwekewa silaha aina ya pisto na dawa za kulevya, ambavyo hakuwa navyo awali.

Pia, alidai alipokamatwa alipewa mateso wakati anasafirishwa kutoka Rao Madukani kwenda katika Kituo cha Polisi cha Kati mkoani Moshi.

Kasekwa alidai kuwa, alisaini karatasi iliyokuwa na maelezo ya onyo yamayodaiwa kuwa ya kwake, baada ya kutishwa bila kupewa nafasi ya kusoma kilichomo ndani yake.

Kwa sasa shahidi wa pili katika kesi hiyo ndogo, Mohammed Abdillah Ling’wenya ameanza kutoa ushahidi wake.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online, MwanaHALISI TV na mitandao yetu kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!