Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mshituko Freeman Mbowe kung’atuka Chadema
Habari za SiasaTangulizi

Mshituko Freeman Mbowe kung’atuka Chadema

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ametamka bayana kuwa anatamani kung’atuka mwaka 2023 na kupisha wengine. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tabora … (endelea).

Uamuzi wa Mbowe kutogombea tena uenyekiti, unaweza kuwa mshituko kwa wanachama na wafuasi wa Chadema, lakini furaha kwa wapinzani wao kisiasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wamekuwa wakipiga kelele kwamba Mbowe hataki kuachia madaraka.

Taarifa kutoka ndani ya Chadema, zimeeleza kumekuwa na mjadala miongoni mwa wanachama kuhusu kauli ya Mbowe kutaka kung’atuka uongozi ifikapo mwaka 2023.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Mbowe kusema hivyo kwani hata katika uchaguzi mkuu wa ndani ya Chadema uliopita mwaka jana, alisema hatagombea, lakini dakika za mwisho alichukuliwa fomu kwa madai amelazimishwa na wazee wa Chadema.

Mbowe alitoa kauli hiyo juzi jumamosi tarehe 5 Juni 2021, akiwa mjini hapa akizungumza kwenye Baraza la Ushauriano la Mkoa wa Tabora na kusisitiza ni vema sasa wanaowania nafasi yake hiyo wakaanza ‘kupasha’.

Alisema uchaguzi mkuu wa chama hicho utafanyika mwaka 2023, hivyo kila mtu ajipange kwa uchaguzi huo, kwa kuwa amekwishakitumikia chama kwa miaka mingi na anadhani imetosha na kubaki kuwa mlezi na mshauri.

Akihutubia wajumbe wa kamati tendaji za Kanda ya Magharibi, Mbowe pia aliwataka wanachama na viongozi, kutambua kushindwa kwao katika uchaguzi mkuu mwaka jana, hakujachangiwa na Hayati Rais John Pombe Magufuli pekee, bali pia ni pamoja na uzembe wao wenyewe.

Kanda ya Magharibi inaundwa na mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.

Alisema hakuna haja ya kumsingizia Hayati Magufuli kuchangia kushindwa kwao, bali nao walihusika kwa kutokuwa makini katika mambo ya msingi, ikiwamo kutojipanga vizuri, kukosa wagombea wenye sifa na kukubalika, wapiga kura wenye sifa.

“Jamani tusimsingizie mwendazake katumaliza, hata sisi wenyewe tulichangia kushindwa, na nataka kuanzia sasa tujipange na tutakuwa na usajili wa wanachama, na kulipia ada kidigitali, kwa sababu tumegundua wenzetu walitupiga kisayansi hivyo nasi lazima tujipange,” alisema

Alisema ili chama kiwe imara na endelevu, kinahitaji viongozi bora, wagombea bora wanaokubalika, kuwa na ajenda inayokubalika na kutambulika, kuwa na mpangilio na rasilimali fedha za kujiendesha, na ndiyo maana wameona waendeshe mambo yao kisayansi zaidi.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Aongoza awamu nne

Mbowe ambaye ni mmoja wa waasisi wa Chadema, amekuwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa kwa vipindi vinne.

Aligombea mara ya kwanza mwaka 2004, na kushinda akimpokea Bob Makani ambaye aliongoza kuanzia mwaka 1999.

Baada ya kuwa Mwenyekiti wa Chadema, alifanya mabadiliko makubwa ndani ya chama.

Ni kipindi hiki Mbowe alianza kutembelea vyuo vikuu nchini, kufuatilia wanasiasa kutoka CCM, NCCR-Mageuzi, CUF, TLP na vyama vingine.

Mmoja wa vijana aliowavuna vyuo vikuu ni pamoja na John Mnyika ambaye sasa ni Katibu Mkuu (Chadema). Pia aliwanasa Zitto Kabwe na Halima Mdee.

Ni katika kipindi hicho, alimnasa pia Tundu Lissu ambaye alikuwa NCCR-Mageuzi.

Wengine waliojiunga Chadema kipindi cha uongozi wa Mbowe kuanzia mwaka 2004 ni pamoja na Profesa Mwesigwa Baregu, Livingstone Lusinde (alirudi CCM na sasa ni Mbunge wa Mtera), Mchungaji Peter Msigwa kutoka TLP, David Silinde na wengine wengi.

Mchungaji Peter Msigwa

Mwaka 2009, Mbowe aligombea tena uenyekiti Chadema ambapo pia aliasisi operesheni mbalimbali ikiwamo maarufu ya Operesheni Sangara Kanda ya Ziwa, ambayo ilimhusisha Katibu Mkuu wa wakati hio, Dk Wilbrod Slaa, Mnyika kama Mkurugenzi wa Vijana, Zitto na viongozi mbalimbali.

Operesheni zingine za kichama zilizofanyika chini ya Mbowe ni ‘Vuvuvugu la Mabadiliko (M4C)’, ‘CHADEMA ni Msingi’ na ‘Pamoja Daima’.

Septemba 14, 2014, Mbowe aligombea tena uenyekiti wa CHADEMA akipambana na Gambaranyere Mwagateka. Katika uchaguzi huo, Mbowe aliibuka mshindi kwa kura 789 huku mpinzani wake akijipatia kura 20.

Mbowe akagombea tena uenyekiti Chadema Agosti 4, mwaka jana, katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, huku Lissu akichaguliwa kuwa Makamu wake upande wa bara bila kuwa nchini.

Uchaguzi huo ulikuwa na sarakasi nyingi, kwani ndio uliosababisha Frederick Sumaye, Waziri Mkuu mstaafu kung’oka Chadema pamoja na Cecil Mwambi, ambao pia walichukua fomu kuwania kiti hicho.

Urais

Mwaka 2005, Mbowe aligombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa na mgombea mwenza kutoka Zanzibar, Jumbe Rajab Jumbe ambaye alifariki dunia, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike Oktoba 30 na hivyo kuahirishwa hadi Desemba 14, 2005.

CHADEMA ilimteua mgombea mwenza Anna Maulid Komu kuwa mgombea mwenza wake wa urais. Hata hivyo, Mbowe alishindwa na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Jakaya Mrisho Kikwete.

Kusajili kidijitali

Katika mkutano wa Tabora juzi, Mbowe ambaye alipata kuwa Mbunge wa Hai kwa vipindi viwili, alisema kuanzia sasa, wanachama watasajiliwa kwa mfumo wa kidigitali, na watalipia ada kwa mfumo huo.

Alisema wanachama wa kawaida watatozwa Sh 2,500 kwa mwaka na atakayehamasisha kupata wanachama kujisajili na kulipa ada atapata Sh 500 kwa kila mwanachama kama kifuta jasho.

Alisema watakuwa pia na kadi za wanachama wa viwango tofauti na wa kawaida, kama wa kadi za bluu za Sh 10,000 kwa mwaka, za fedha Sh 25,000, za dhahabu Sh 50,000, za platinamu Sh 100,000 na za almasi Sh 200,000 ambazo wanaweza kulipia kuanzia mwaka hadi miaka mitano.

Freeman Aikaeli Mbowe, alizaliwa tarehe 14 Septemba 1961, mwaka ambao Tanganyika ilipata uhuru wake na sasa ana miaka 59.

Ikiwa mwaka 2023 atang’atuka kama alivyosema, atakuwa na miaka 61 huku akiwa amekifanya chama hicho kukuwa na kusambaa nchi nzima.

Kabla ya Mbowe kuingia kwenye siasa mwaka 1992, alifanya kazi Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kama Afisa wa Benki Kuu akiwa chini ya Edwin Mtei na Bob Makani, ambaye kwa sasa ni marehemu.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaKimataifa

Mwanaye rais jela miaka miaka 6 kwa dawa za kulevya

Spread the loveMwanawe rais wa zamani wa Guinea-Bissau amehukumiwa kifungo cha miaka...

Habari za SiasaTangulizi

Mapya yaibuka wamasai waliohamishwa Ngorongoro kwenda Msomera

Spread the loveMAPYA yameibuka kuhusu zoezi la Serikali kuwahamisha kwa hiari wamasai...

Habari MchanganyikoTangulizi

Baba aomba msaada kuzika miili ya familia yake iliyofunga bila kula kuonana na Mungu

Spread the loveWAKATI Mamlaka nchini Kenya, ikiendelea kukabidhi miili ya watu waliofariki...

Habari za Siasa

Rais Samia ampongeza mpinzani aliyeshinda urais Senegal

Spread the loveRAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amempongeza mwanasiasa wa...

error: Content is protected !!