June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mshindo wa Lowassa hadharani

Spread the love

NGUVU ya utendaji kazi kimkakati iliyopo Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) inatarajiwa kudhihiri kesho utakaposhuhudiwa uzinduzi rasmi wa kampeni yake ya kushika hatamu za uongozi wa nchi. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Ni kesho umma wa Watanzania uliojaa shauku ya mabadiliko ya mfumo wa uongozi wa jamhuri utaona staili mpya ya kampeni inayoshirikisha mgombea urais anayewakilisha vyama vinne vya siasa.

Itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi mkuu nchini, mgombea kuungwa mkono na kundi la vyama, dhamiri ikiwa kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichothibitisha kuchoka.

Ukawa ni umoja unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

Vyama hivi vilivyounda umoja mwaka 2013, baada ya majadiliano ya muda mrefu vimemteua Edward Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzulu Februari 2008 kwa shinikizo la Bunge, kuwania urais akiwa amehama CCM alikokatwa jina lake kuwania nafasi hiyo, mwenyewe akilalamika amehujumiwa kichuki.

Lowassa anawania wadhifa huo akifuatana na Juma Duni Haji, mwanasiasa shupavu kutoka Zanzibar aliyelazimika kuhama CUF na kujiunga Chadema, kama hatua ya kurahisisha utaratibu wa kisheria wa kugombea.

Duni ndiye mgombea mwenza, ambaye UKAWA ukifanikiwa kushinda uchaguzi wa 25 Oktoba, na hivyo kuunda serikali, atakuwa moja kwa moja makamu wa rais wa jamhuri.

Tangu mfumo wa vyama vingi uliporudishwa nchini kwa sheria ya bunge Juni 1992, ni mara ya kwanza kuwepo mgombea urais anayeungwa mkono na vyama vinne vikiwemo vyenye nguvu na ushawishi unaochangiwa na kuwa na wabunge zaidi ya 100 katika bunge la jamhuri.

Inatarajiwa umoja huo utaongeza idadi ya majimbo hata kudhibiti bunge na iwapo watapata urais, itakuwa wameondoa mfumo mbaya wa uongozi uliodumu kwa zaidi ya miaka 50.

Nguvu hiyo ya vyama vinne, ndiyo imesababisha taharuki ndani ya mfumo wa utawala wa nchi unaoongozwa na CCM, chama ambacho kimefika mwisho wa uwezo wa kupambana na maadui watatu wakuu nchini – njaa, ujinga na maradhi – na kujikuta ikizidiwa na matatizo mengine makubwa yanayovuta uchumi usikue katika kiwango kinachomnufaisha mwananchi wa chini.

Serikali ya CCM inakabiliwa na lawama nyingi za kulea mfumo wa kufuja mali za umma zikiwemo raslimali za nchi, kutokana na kukithiri kwa rushwa, ufisadi na uzembe serikalini.

Lowassa na Duni wanatarajiwa kutoa mkakati mahsusi wa kuiondoa nchi na matatizo hayo kufuatana na manifesto (Ilani ya Uchaguzi) ya pamoja iliyobuniwa na timu ya wataalamu ya Ukawa.

Uzinduzi rasmi wa kampeni unafanyika ndani ya wingu la visa na vituko vilivyoshuhudiwa vikipaliliwa na vyombo vya dola hasahasa Jeshi la Polisi linaloingia hata kujaribu kupanga wao utaratibu wa kampeni badala ya vyama vyenyewe.

Tayari jeshi hilo limetoa amri kadhaa za kukwaza mwenendo wa kampeni mara tu baada ya Lowassa na Duni kujishusha chini waliko wananchi wa kawaida kujifunza matatizo yanayowakabili.

Walianza kutumia usafiri wa umma (daladala) kati ya Gongo la Mboto na Mbagala, na kupokewa na umma mkubwa wa wananchi walioeleza shida zinazowakabili. Hata wanafunzi walipata nafasi ya kueleza wanavyopata wakati mgumu kuhudhuria shule kwa shida ya usafiri.

Siku ya pili, wagombea hao walitembelea masoko ya mitaani kama Tandale na tandika, lakini ghafla akaibuka Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na kuwazuia wasiendelee na utaratibu huo.

Wakati Lowassa na Duni wanazuiwa, mgombea wa CCM, John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan, wanaendelea kuzunguka nchi ikiwemo kuingia hadi kwenye wodi za wagonjwa bila ya kuzuiwa.

error: Content is protected !!