July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mshindo wa CUF Z’bar

Spread the love

KIMYA cha viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kina mshindo visiwani Zanzibar, hata hivyo chama hicho kinasema kinapambana na sera za kibabe za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Regina Mkonde.

Kinaeleza kuwa, umoja na mshikamano wa wapenda haki hasa katika kipindi hiki cha mgogoro wa kisiasa ndio njia pekee ya kuhakikisha sera haramu na za kibabe zinazikwa visiwani humo.

Shaweji Mketo, Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu Taifa amesema, CUF na Watanzania sasa wanaelewa kwamba, kwa Serikali ya CCM hoja si haki isipokuwa kupata kile wanachokitaka.

Akizungumza na mtandao huu leo kwenye Ofisi Kuu ya CUF amesema, CCM haifuati sheria na imejikita katika kukandamiza uhuru na demokrasia huku utafutaji wa suluhu ukiwa ni wa mabavu.

“Mambo mengi yanayofanywa na serikali hayafuati sheria na misingi ya demokrasia, hufanya mambo kwa kulinda maslahi ya chama tawala hata kama wanajua wanavunja sheria,” amesema Mketo.

Ametaja baadhi ya mambo ambayo yanaviashiria vya uvunjwaji wa sheria na ukandamizaji wa demokrasia kuwa ni pamoja na kulazimisha vyama vya siasa kufuata matakwa yao pia Jeshi la Polisi kutotendea haki vyama vya upinzani.

“Kufutwa na kurudiwa kwa uchaguzi visiwani Zanzibar bila ya sababu za msingi ni kuikandamiza demokrasia na kukiuka sheria, kama uchaguzi haukuwa wa haki, nani aliyeipoteza haki?” amehoji Mketo na kuongeza;

“Hata siku moja chama cha upinzani hakitafanikiwa kuiba kura, sababu Tume na watendaji wake huchaguliwa na Rais ambaye anatoka chama tawala.

“Ili wapinzani waibe kura inabidi washirikiane na Tume ambao ni Mwenyekiti, Wakurugenzi na Makamishina, wote wamechaguliwa na Rais, kwa hiyo si rahisi kuwarubuni,” amesema.

Mketo amedai kuwa, chaguzi nyingi zilizopita mgombea wa CUF alikuwa ni mshindi lakini waliminya demokrasia kwa Tume kumpitisha wanayemtaka, pia ametoa mfano wa uchaguzi uliofanyika mwaka 1995.

“Uchaguzi wa mwaka 1995, mgombea wa upinzani alipita, kituo cha televisheni cha DTV ambacho sasa ni Chanel Ten, kilifungiwa baada ya kutangaza kuwa Maalim Seif aongoza Zanzibar,” amesema.

Mketo amesema, wagombea wote wa CUF wameiandikia barua tume ya ZEC na viapo ili kuwaeleza kwamba, hawatashiriki katika uchaguzi wa marudio.

“Hata kama ZEC ikilazimisha kuweka jina la Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF na ikaonekana ameshinda, Maalim Seif hatokubali kuichukua nchi, sababu ameshakataa kurudiwa kwa uchaguzi,” amesema na kuongeza;

“Wananchi wengi wa Zanzibar hawakubali kurudia uchaguzi, wanaijua demokrasi na haki yao, hawatapiga kura sababu viongozi wanaowataka, wameshawachagua.”

Kuhusu kuzuiliwa kwa maandamano ya Jumuiya ya Wanawake CUF-Taifa amesema, kitendo cha polisi kuwanyima kibali ni kinyume cha sheria na walikifanya hivyo ili kulinda masilahi ya serikali.

“Kwa mujibu wa sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya 1992, imetoa haki kwa vyama vya siasa kuandamana na inasema vyama vinatakiwa kutoa taarifa ya maandamano kabla ya siku mbili,” amesema Mketo.

error: Content is protected !!