August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mshahara wa Oscar kuwafunika Messi, Ronaldo

Spread the love

KIUNGO wa Chelsea na timu ya taifa ya Brazil Oscar do Santos huenda akawa mchezaji anayelipwa kiasi kikubwa cha fedha kuliko wote duniani ikiwa atakamilisha uhamisho na kutua katika klabu ya Shanghai SIPG inayoshiriki ligi kuu nchini china wakati wa dirisha dogo la usajili, anaandika Kelvin Mwaipungu.

Klabu hiyo ipo tayari kuilipa Chelsea Pauni milioni 60 ili kumnasa kiungo huyo huku ikiwa tayari kumlipa mshahara mnono wa Pauni 400,000 kwa wiki ambazo ni sawa na Pauni milioni 20.8 kwa mwaka na kumfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi duniani.

Oscar amekosa nafasi ya uhakika ndani ya kikosi cha kocha muitaliano Antonio Conte, kinachoongoza ligi kuu ya Uingereza kwa sasa huku kikiwa kimeshinda michezo 10 mfululizo iliyopita.

Iwapo atatua katika klabu ya Shanghai SIPG, Oscar atakutana tena na aliyekuwa meneja wake wa zamani wa klabu Chelsea, Mreno Andre Villas-Boas (AVB), ambaye kwa sasa ndiye kocha wa klabu hiyo ya nchini China.

Mbali na kumuhitaji Oscar, klabu hiyo pia ipo katika mipango wa kumchukua nyota wa zamani wa Manchester united na Manchester City Carlos Tevez ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Boca Juniors.

China kwa sasa inajaribu kuwekeza kwenye soko la mpira wa miguu duniani, klabu nyingi za nchini humo zinajiandaa kulipa pesa nyingi kwa kununua wachzaji wengi wazuri na wenye majina makubwa kwenye dirisha dogo la usajili mwezi Januari, 2017.

Kwa sasa nyota wawili wanaotamba zaidi duniani Lionel Messi wa Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid wanapokea mishahara iliyo chini ya pauni 400,000 kwa wiki ambayo Oscar anatarajia kupokea katika klabu ya Shanghai.

Takwimu zinaonesha kuwa Messi anapokea kiasi cha Pauni 350,000 kwa wiki huku Ronaldo akipokea Pauni 360,000 kwa wiki.

error: Content is protected !!