January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msekwa: Hatutajali umaarufu kumpata mgombea urais CCM

Viongozi wa CCM wakiwa katika kikao cha maamuzi

Spread the love

KADA Mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa amesema, chama hicho hakitampitisha mgombea urais kwa sababu ya umaarufu wake tu. Anaandika  Jimmy Mfuru … (endelea).

Msekwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Chama (CCM) amesema, mgombea atakayepitishwa na chama hicho ni yule mwenye kukubalika kimaadili pekee.

“Uteuzi hautakuwa mgumu kumpata mgombea. Tutatumia sheria, kanuni, taratibu na vigezo na tutampata mtu anayekubalika kimaadili na si anayependwa na watu,” amesema Msekwa.

Amesema, katika kuhakikisha wanampata mtu sahihi licha ya utitiri wa makada wengi kuomba nafasi hiyo nyeti, watatumia kanuni, sheria na taratibu hizo zilizowekwa.

Mpaka sasa makada ambao waliomba kuteuliwa na chama hicho katika kukiwakilisha kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, waliorejesha fomu hizo ni 38, wanne wakishindwa kurejesha.

“Haki na usawa bila upendeleo wowote ni sehemu muhimu ili kumpata gombea huyo,” amesema Msekwa ambaye ni Spika Mstaafu wa Bunge  amesema hayo leo alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia maadili amesema ili kuhakikisha wanayarejesha kwa makada wao baada ya kushuka, wameanzisha Kitengo cha  Kibweta cha Mwalimu Nyerere katika Chuo Cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kivukoni jijini Dar es Salaam na kwamba,  tayari makada wapatao 40 wameshaanza kunolewa chuoni hapo ili kurejesha heshima.

“Hali siyo nzuri, maadili kwa viongozi yameporomoka, wengi wamekuwa na skendo. Ni tabia isiyopendeza kwao hivyo kuanzisha kwa kitengo hiki kitarejesha maadili kwa viongozi darasa hili litakuwa la miezi mitatu mwezi mmoja darasani na miezi miwili kivitendo,” amesema Msekwa ambaye sasa hivi ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.

Amesema, maadili yamemomonyoka baada ya kuondolewa kwa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana suala ambalo lilikuwa linajenga uzalendo kwa vijana na kuipenda nchi yao.

error: Content is protected !!