July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Msama aingilia kati kazi za wasanii

Spread the love

ALEX Msama, Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion, ameomba kibali cha Jeshi la Polisi kuzunguka nchi nzima kupambana na wezi wa kazi za wasanii, anaandika Dany Tibason.

Pamoja na hivyo, ameiomba serikali kuwasaidia wasanii kwa vitendo badala ya kuwatumia majukwaani pekee.

Amesema, umefika wakati kwa  serikali kuwasaka wezi wa kazi za wasanii kama inavyosaka wahalifu wengine ikiwemo wauzaji wa dawa za kulevya na majangili.

Ametoa kauli hiyo alipozungumza mwandishi wa mtandao huu akieleza kusikitishwa na baadhi ya watu wanaoiba kazi za wasanii kwa kuzaliza CD na DVD  bila kuwa na makubaliano rasmi.

Amesema, kwa sasa wizi wa kazi za wasanii umeibuka mara mbili zaidi ya hapo awali jambo ambalo linawafanya wasanii kukosa mapato ambayo yanatokana na jasho lao.

Kutokana na hilo amesema, kwa sasa ameomba kibali cha polisi kwa ajili ya kuanza msako kwa  wezi wa kazi za wasanii ambao aliwaita manyang’au.

Amesema, kazi ya kupambana na wezi wa kazi za wasanii siyo ya mtu mmoja bali serikali inatakiwa kuweka mkono wake.

“Kwa sasa naomba kibali kutoka polisi kwa ajili ya kuzunguka nchi nzima na safari hii nitaenda hadi vitongoji.

“Japo kazi hii siyo ndogo na inanijengea uhasama mkubwa na watu lakini hakuna jinsi lazima nipambane ili kazi za wasanii zilindwe na ziheshimiwe,” amesema Msama.

 

error: Content is protected !!