September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Jaji Mutungi, kuwakutanisha IGP Siro na viongozi wa vyama vya siasa

Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania

Spread the love

 

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi, ameitisha mkutano wa pamoja kati ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro. Anaripoti Anaripoti Gabriel Mushi, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Jumatatu tarehe 6 Septemba, jijini Dar es Salaam, Jaji Mutungi alisema, Polisi ndio wanaosimamia mikutano ya vyama vya siasa, kwa maana ya kutoa ulinzi, hivyo ametaka kiongozi huyo na wale wa vyama kukutana, ili kukubaliana namna bora ya kutelekeza jambo hilo.

Alisema, tayari amekutana na IGP Sirro na kukubaliana kuwapo kwa mkutano huo, ambao hata hivyo, hakueleza utafanyika lini.

Jaji Mutungi amesema, ameshtushwa na kitendo cha polisi kujazana na mabomu katika kila mikutano ya vyama vya siasa, jambo ambalo amedai kuwa linaleta taswira hasi, kwamba hali ya kisiasa nchini siyo shwari.

Amesema, “malengo ya mkutano huo utakaotishwa hivi karibuni na IGP Sirro, ni kujadili kuhusu namna bora ya vyama vya siasa kutimiza majukumu ya kisheria, ikiwamo mikutano ya ndani na ile ya hadhara. Tunataka jambo hili lijadiliwe mezani na kupatikana muafaka wa pamoja.”

Ameongeza, “tumekubaliana na IGP Sirro kuitisha kikao na wadau wa siasa, ili kujadili na kufikia muafaka kuhusu mtafaruku wa sitisho la mikutano ya hadhara na ya ndani nchini.”

Aidha, Msajili wa Vyama amewaomba viongozi wa vyama vya siasa, kusitisha kwa muda mikutano yao ya ndani na ile ya hadhara, pamoja na makongamano waliyopanga kuyatekeleza, hadi mkutano kati yao na IGP utakapofanyika.

Amesema, ameamua kuchukua hatua hiyo, ili kuhakikisha mfumo wa vyama vingi unaendelea kuimarisha nchini na kuondoa manung’uniko miongoni mwa wadaau wa siasa.

error: Content is protected !!