June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msaidizi wa IGP na familia yake aagwa Dodoma

Spread the love

MKUU  wa Mkoa wa Dodoma luteni mstaafu Chiku Galawa ameongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma na maofisa wa jeshi la polisi kuaga miili ya familia ya marehemu Inspekta, Gerald Ryoba aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi Polisi (IGP), Ernest Mangu. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Januari 3 mwaka huu Msaidizi huyo alifariki na familia yake, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji ya mafuriko katika eneo la Kibaigwa bwawani wilaya ya Kongwa Mkoani hapa.

Aidha familia ya marehemu Gerald ilikuwa ikitokea likizo mkoani Geita kuelekea jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea kutokana na mvua kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali na kujikusana katika mkondo wa maji na kupelekea kuziba barabara.

Mvua hizo kubwa zilinyesha  maeneo ya kiteto kutiririsha maji yaliyokuwa na kasi kubwa kwenye barabara kuu ya Dodoma-Morogoro na kusomba gari walilokuwa wakisafiria familia hiyo.

Akiongoza waombolezaji hao mkuu wa mkoa wa Dodoma, Galawa akitoa salamu kwa waombolezaji amesema jeshi la polisi na taifa kwa ujumla limepata pigo kubwa kumpoteza msaidizi wa IGP.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime amesema marehemu Ryoba enzi za uhai wake alikuwa ni kiunganishi kikubwa kwa askari wa vyeo vyote.

Misime amesema marehemu aliweza kuwaunganisha askari na viongozi wa  ngazi ya juu ambayo ni IGP  na makamishna wa jeshi hilo na pengo lake kiutendaji litachukua muda mrefu kusahaulika.

Awali Mchungaji wa Anglikana, Yohana Chisoma akifanya ibada ya kuwaombea marehemu  hao  amewakumbusha waombolezaji kuwa maisha ya mwanadamu duniani ni mafupi na hakuna ambaye anajua siku yake ya kuondoka duniani.

Amesema ni vyema watu wakatambua wajibu wao na kutenda yaliyo mema siku zote kama ambayo maandiko yanaagiza.

error: Content is protected !!