January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msafara wa Mgombea wa Chadema wapigwa mabomu

Spread the love

MJI wa Musoma mkoani Mara, jana uligeuka uwanja wa kivita baada ya Askari Polisi waliokuwa na silaha za moto kuanza kupiga mabomu ya machozi hewani katika msafara wa mgombea ubunge jimbo la Musoma Mjini, Vicent Nyerere (Chadema). Anaandika Moses Mseti, Musoma … (endelea).

Tukio hilo lilitokea saa 1:15 jioni wakati msafara huo, ulipokuwa ukitokea katika mkutano wa hadhara ambako kulikuwa na uzinduzi wa kampeni za mgombea udiwani kata ya Lwamlimi, Joseph Kani.

Katika msafara huo uliokuwa ukiongozwa na Nyerere pamoja na mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini, John Heche, ulionekana kuungwa mkono na vijana, wanawake na wazee ambao waliokuwa wakitembea kwa miguu.

Hata hivyo msafara huo uliokuwa ukitokea katika uwanja wa Shule ya Msingi Lwamlimi na ulipofika katika eneo Mkendo, Askari polisi hao walianza kupiga mabomu juu kitendo ambacho kilisababisha watoto na wanawake waliokuwa katika maandamano hayo ya kuwasindikiza viongozi hao kukimbilia kusikojulikana.

Katika kile kilichoonekana wananchi na wafuasi wa chama hicho kutokukubaliana na vitendo vya jeshi la Polisi kuwanyanyasa kwa kuwapiga mabomu kwa lengo la kuwatawanya, waliendelea kukusanyika katika vikundi na kuanza safari hadi Ofisi za Chadema zilizopo eneo uhindini.

Akizungumzia tukio hilo, Nyerere ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Mara, amelitupia lawama jeshi la Polisi kugeuka mawakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huu wa Oktoba 25.

Amesema Polisi wamekuwa watumishi na mawakala wa CCM na wameshindwa kulinda raia na mali zao kitendo ambacho kinaonesha taasisi hiyo ni ya chama tawala na sio ya wananchi wote ambao wanawalipa mishahara.

“Nashindwa kuelewa ni kwanini hawa Polisi wapige mabomu kwenye mikutano ya Chadema na maandamano yao, CCM wao wakiandamana hawapigwi mabomu, ukiangalia maandamo yalikuwa ni ya kutusindikiza sisi viongozi,” amesema Nyerere.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philip Kalangi, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo kupitia simu yake ya mkononi, amesema kuwa hayupo tayari kutoa taarifa hizo na alipofuatwa ofisini alikataa kuzungumza bila sababu za msingi.

“Sipo tayari kukupa habari hizi na kamwambie mhariri wako kwamba na nimekataa kukupa habari, wewe ni mwandishi sikupi taarifa,” amesema Kalangi bila kuainisha sababu za kushindwa kutoa taarifa hizo.

Hata hivyo jeshi Polisi Mkoa wa Mara, limekuwa likilalamikiwa na wananchi kwamba limekuwa likiwabambikizia kesi na kuwanyanyasa hali ambayo wananchi kudai kuichoka taasisi hiyo na wakuu wa Polisi wakishindwa kuchukua hatua zozote.

error: Content is protected !!