MSAFARA wa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, uliokuwa njiani kuelekea Mkoa wa Kusini Unguja kwa ziara ya kikazi, umepata ajali huku mtu mmoja akifariki dunia. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa zinaeleza, aliyefariki dunia ni Hamis Machenga, aliyekuwa mhudumu wa habari katika ofisi ya makamu wa pili wa rais ambapo watatu wamejeruhiwa.
Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kusini Unguja, Suleiman Hassan Suleiman, amesema ajali hiyo imetokea asubui ya leo Jumatano tarehe 10 Machi 2021.
Alipoulizwa juu ya taarifa za majeruhi wa ajali hiyo, Kamanda Suleiman amesema, taarifa kamili atazitooa baadaye.
“Ni kweli ajali hiyo imetokea lakini sina taarifa zaidi kuhusu ajali hiyo, naendelea kufuatilia, nitatoa taarifa baadaye,” amesema Kamanda Suleiman.
Hata hivyo, taarifa za awali zinaeleza kwamba walioathirika katika ajali hiyo ni wanahabari ikiwemo maofisa wa kitengo cha habari cha Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, baada ya gari yao kupinduka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kituo cha Televisheni cha ITV, ajali hiyo imesababisha kifo cha Hamis Machenga, aliyekuwa mhudumu wa habari katika ofisi hiyo, na kujeruhi watu takribani wanne waliokuwa katika gari hiyo.
Taarifa hiyo ya ITV imesema kuwa, Machenga alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja iliyoko Unguja, Zanzibar.
Pia, majeruhi wanaendelea na matibabu hospitalini hapo kutokana na majerah mbalimbali waliyopata, kwenye ajali hiyo.
Chanzo cha ajali hiyo kinadaiwa kuwa, gari ya raia wa kigeni kuingilia msafara huo na kuigonga gari iliyobeba waandishi kisha kusababisha gari hiyo kupinduka.
Leave a comment