September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mrundikano mahabusu wazua mjadala bungeni, Spika Ndugai atoa agizo

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amewataka wabunge wasitunge sheria zinazoongeza changamoto ya mrundikano wa mahabusu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Spika Ndugai ametoa agizo hilo leo Jumatatu, tarehe 6 Septemba 2021, bungeni jijini Dodoma, baada ya baadhi ya wabunge kuibua mjadala, kuhusu changamoto ya mrundikano wa mahabusu nchini.

“Wabunge na sisi kupitia kamati zetu mbalimbali tuangalie na sisi mchango wetu katika jambo hili, kila tunapotunga sheria si kuna adhabu kule mbele? Kufunga watu miaka 20, 15 ngapi, dunia ya leo ilivyofasta ukimfunga mtu mwaka yaani kama mtu wa kurebebika anarekebika sana,” amesema Spika Ndugai na kuongeza:

“Sasa hivi tuangalie na sisi tunapotunga sheria zetu na sisi ni sehemu ya sababu ya mrundikano wa wafungwa kwa namna moja au nyingine. Kwa namna ambavyo tunatunga aina ya adhabu zetu na sisi tubadilike kidogo tuangalie.”

Mjadala huo uliibuka baada ya Mbunge Viti Maalum (CCM), Neema Lugangira, kuhoji kwa nini mahakama isipewe jukumu la kugharamia chakula cha mahabusu walioko gerezani, kutokana na ucheleweshaji wa hukumu ya kesi.

Lugangira alijibiwa swali hilo na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda, aliyesema jukumu la kusimamia chakula cha wafungwa linasimamiwa na Mkuu wa Magereza kwa mujibu wa sheria.

“Mahakama haijawahi kuchelewesha utoaji wa maamuzi ya mashauri mbalimbali bila uwepo wasababu muhimu zinazochangia kuchelewa kwa kesi husika. Wote tunafahamu kuwa vipo vyombo mbalimbali vinavyohusika katika suala la kesi,” alisema Pinda.

Alisema “hivyo katika sura ya kawaida huonekana kuwa mahakama ndiyo zinazochelewesha utoaji wa hukumu, lakini ukweli ni kwamba kesi huchakatwa na vyombo nilivyovitaja na wakati mwingine mchakato huchukua muda mrefu kabla ya kutoa nafasi kwa Mahakama kutolea maamuzi.”

Baada ya Pinda kutoa majibu hayo, Mbunge Viti Maalum asiye na chama bungeni, Halima Mdee, alimhoji naibu waziri huyo kwamba, ni sahihi kesi kucheleweshwa kutokana na taratibu zinazoendeshwa na vyombo hivyo.

“Waziri wakati anajibu swali alisema kwamba kesi zinachelewa sababu vyombo mbalimbali vinachakata, nimuulzie waziri vyombo kuendelea kuchakata wakati watu wako magereza uandhani ni sawa?”

“Na kama sio sawa unadhani badala ya kutoa maagizo bungeni, ni wakati muafaka kwa Serikali kufanya kazi ya ziada kwenda kuchunguza kinaga ubaga ili kuja na majibu ambayo yatasaidia wananchi,” amesema Mdee.

Akijibu swali hilo, Pinda amesema Serikali imeshaanza kufanya uchunguzi wa changamoto hiyo na kwamba kuna baadhi ya mahabusu ambao kesi zao hazina mashiko wameanza kuachwa huru.

Naye Mbunge Viti Maalum asiye na chama bungeni, Esther Matiko, alihoji kwa nini watuhumiwa wasifikishwe mahakamani baada ya upelelezi wa makosa yao kukamilika ili kuondoa mrundikano wa mahabusu.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene alitoa wito kwa vyombo vya kisheria kutoa dhamana kwa watuhumiwa ambao makosa yao yana dahamana, huku akiwataka watu wenye taarifa za mahabusu wanaonyimwa dhamana kinyume cha sheria kuzitoa ili zifanyiwe kazi.

error: Content is protected !!