August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF kumchagua mrithi wa Prof. Lipumba

Spread the love

MAJINA matatu ya wanachama wanaowania nafasi ya mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) iliyoachwa wazi kufuatia kujiuzulu ghafla kwa Profesa Ibrahim Lipumba mapema Agosti mwaka jana, yametajwa, anaandika Pendo Omary.

Katika majina hayo, limo la Twaha Issa Taslima, wakili wa Mahakama Kuu nchini aliyeongoza kamati ya watu watatu kushikilia uenyekiti hadi utakapofanyika mkutano mkuu maalum wa kuchagua kiongozi mpya. Anashirikiana na Abubakar Khamis Bakary na Severine Mwijage.

Majina yaliyobaki ni ya Juma Nkumbi, Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, na Riziki Shahari Ngwali, Mbunge wa Viti Maalum kutokea wilayani Mafia, mkoani Pwani. Huyu pia ni kiongozi wa wabunge wa CUF.

Majina hayo yamepitishwa na Baraza Kuu la Uongozi (BKUT) lililoketi jana kujadili majina ya waombaji tisa yatakayofikishwa mbele ya mkutano mkuu maalum unaofanyika mchana huu ndani ya Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Mkutano huo unaohudhuriwa na wajumbe 832, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Shaweji Mketo, pia utamchagua makamu mwenyekiti mpya kujaza nafasi iliyoachwa tangu kabla ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani ambapo Juma Duni Haji aliridhiwa kujiuzulu ili kuwania umakamu wa rais akibebwa na Edward Lowassa aliyegombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Lowassa alikuwa amekihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kabla kilimkata kihujuma Lowassa katika orodha ya wawaniaji urais na hivyo kuzusha malalamiko ambayo hatimaye yamekipasua chama hicho.

Baraza Kuu la CUF ambalo pia limejadili na kupitia majina wanachama 34 wanaowania za ujumbe wa baraza hilo, limewapeleka mbele ya mkutano mkuu maalum viongozi wake waandamizi Salim Abdalla Bimani na Mussa Haji Kombo wanaowania umakamu mwenyekiti.

Bimani na Kombo wamebaki baada ya wawaniaji wenzao awali, Dk. Juma Ameir Muchi na Juma Duni Haji, kujitoa mapema. Sababu za kujitoa kwao hazijaelezwa ingawa imetajwa kuwa Duni amehofia kukivuruga chama baada ya kubainika kuwepo kundi la wanachama walioazimia kumpinga mahakamani akichaguliwa.

Mketo amewaambia waandishi wa habari mapema leo kuwa Duni amejitoa ili kulinda maslahi ya chama kwa kuwa wanaomlalamikia wanatumia kifungu cha Katiba ya chama hicho kinachozuia mwanachama aliyekihama chama kugombea uongozi mpaka atimize miaka miwili.

Chama hicho kilimuidhinisha Duni kuondoka baada ya kufanya makubaliano na Chadema pamoja na NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD) ya kuwezesha ushirikiano wao chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kusimamisha mgombea mmoja kwenye uchaguzi mkuu wa taifa.

UKAWA waliendesha walifanya kampeni maridadi lakini matumaini yao ya kutwaa madaraka yalizimwa kutokana na walichoita “mbinu kali” za CCM zilizolenga kukiwezesha kubaki madarakani. Mpaka sasa Lowassa na UKAWA wanamsimamo kuwa ushindi wao ulihujumiwa.

Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa leo jioni.

…………………………………………………………………………………………………..

Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia (bonyeza)> Simgazeti kwa wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel. Pia unaweza kupakua (download) app ya Mpaper au Simgazeti kutoka kwenye playstore.

error: Content is protected !!