August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mrithi wa Dk. Dau huyu hapa

Spread the love

HATIMAYE Rais John Magufuli amefanya uteuzi wa nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambapo Profesa Godius Kahyarara ameteuliwa kushika nafasi hiyo, anaandika Charles William.

Pamoja na hivyo Rais Magufuli amemteua Dk. Ayub Rioba kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) ambapo Dk. Mussa Mgwatu ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO).

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam imearifu kuwa Rais Magufuli amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo.

Prof. Kahyarara amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Ramadhan Dau ambaye kwa sasa anasubiri kupangiwa uwakilishi wa nchi (ubalozi).

Prof. Kahyarara ni mchumi mbobezi kitaaluma na ndiye Mkuu wa Chuo cha Sayansi ya Jamii (COSS) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Dk. Rioba Mkurugenzi mpya wa TBC alikuwa Mkuu wa Shule Kuu ya Habari na Mawasiliano kwa Umma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Clement Mshana ambaye amefikisha umri wa kustaafu.

Dk. Mgwatu Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhandisi Benhadard Tito, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa kutokana na utendaji usioridhisha.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Gerson Msigwa, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, imearifu kuwa uteuzi huo unaanza kazi mara moja baada ya kutangazwa.

 

error: Content is protected !!