July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mrema: Rais Magufuli atanitafutia kazi

Spread the love

AUGUSTINE Mrema, Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labor Party (TLP) Taifa na aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Vunjo mkoani Kilimnjaro katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana bado ana ndoto za kupewa kazi na Rais John Magufuli, Anaandika Regina Mkonde.

Mrema amesema kuwa, anamuacha Rais Magufuli kwa muda atekeleze majukumu ya kuisuka nchi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kumuomba kazi anayoitaka.

“Mimi siwezi kupiga ramli kwa sasa, tumuache Rais afanye kazi ya kuitengeneza nchi na chama tawala halafu tutaona atamsaidia wapi Mrema na wakati ukifika nitamnong’oneza nitakachotaka.” Amesema Mrema mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mrema amesema kuwa, TLP kupitia kikao chake cha Sekretarieti kilichokaa 8 Juni, 2016 kinampongeza Rais Magufuli kwa ujasiri wa kumuombea kura yeye aliouonesha mbele ya wananchi wa jimbo la Vunjo.

 

“Licha ya kweli kwamba chama chake (CCM) kilikuwa na mgombea wake kwenye jimbo la Vunjo lakini Magufuli alininadi mimi na kusema hata kama wananchi hawatanichagua yeye akishinda atanipatia kazi.” Amesisitiza Mrema.

Mrema pia amesema, TLP imesikitishwa na kitendo kilichofanywa na baadhi ya vyama vya upinzani kwa kuelekeza nguvu zote kwenye jimbo la Vunjo ambalo tayari ni la upinzani na kuyaacha majimbo mengine yakichukuliwa na CCM.

“Sekretarieti yetu inaona kilichofanywa na baadhi ya vyama vya upinzani ni kinyume na dhana ya umoja na mshikamano kati ya vyama vya upinzani na ni kichocheo cha CCM kuendelea kuwa na wabunge wengi bungeni.” amesema Mrema.

8 Oktoba, 2015 wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu, Dk. Magufuli akiwa mgombea urais wa CCM alilitembelea jimbo la Vunjo na kumuombea kura Mrema huku Mrema naye akimuombea kura Dk. Magufuli.

“Kama hamumtaki Innocent Shirima wa CCM basi angalau mniletee Mrema wa TLP na kama akichaguliwa mgombea wa CCM mimi sitamsahau Mrema, nitamtafutia kazi nyingine.” Alisema Dk. Magufuli.

James Mbatia ndiye aliyeibuka na mshindi wa kiti cha ubunge katika jimbo hilo kwa kupata kura 60,187 dhidi ya kura 16,617 za Innocent Shirima wa CCM huku Augustine Mrema wa TLP akipata kura 6,416.

error: Content is protected !!