July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mrema ajificha kwa Lowassa

Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema akiwa anatafakari bungeni

Spread the love

HATUA ya Augustino Mrema, Mwenyekiti wa Chama cha TLP kutajwa kama wakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani ya upinzani, inamkera, anaandika Regina Mkonde.

Mrema ambaye hivi karibuni Rais John Magufuli ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Parole amesema, yeye si CCM B na kwamba, ikiwa hivyo basi Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mwaka jana, anapaswa kuitwa CCM B.  

“Kama ni hivyo, basi na Lowassa ni CCM B, si alihama mwaka jana,” amesema Mrema leo kwenye mkutano wake na madereva wa bodaboda katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Lowassa alihamia Chadema mwaka 2015 baada ya kuonekana kile kilichoitwa mizengwe ndani ya CCM hasa baada ya jina lake kuondolewa kabla ya kupigiwa kura ya uteuzi wa mgombea ngazi ya urais katika kukiwakilisha chama hichi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Mrema amekuwa akipata wakati mgumu kujitetea pale anapohusishwa na harakati zake za kisiasa kwamba, amekuwa akitumikia CCM zaidi ya upinzani.

“Hata angekuja Lowassa, ningemuuliza mwaka ule nilipofukuzwa nilimwambia tuhamie upinzani wote, akakataa hadi alipojitoa mwaka jana CCM,” amesema na kuongeza;

“Sumaye (Frederick Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu) naye alikuwepo, nilimwambia njoo huku. Waliposhindwa kuteuliwa kuwania urais waliondoka, halafu wanasema mimi ni CCM B, wao nani.?”

Mrema mesema, alilazimika kumpigia kampeni Rais Magufuli katika Uchaguzi kwa imani kuwa, ndiye aliyemuona anafaa.

Katika hatua nyingine, Mrema amempa siku saba Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kumueleza sababu ya madereva wa bodaboda kufanya shughuli zao maeneo ya mjini yaliyokatazwa.

“Natoa siku saba, nataka kujua Makonda hao waliofanya shughuli hizi sehemu zilizokatazwa, wanafanya hivyo kwa niaba ya nani?” amehoji Mrema na kuongeza;

“Makonda nakwambia, kama unajifanya huna macho na huoni, huna masikio na husikii, mbona ukiona majipu unakuwa mwepesi kuyatumbua, kwa nini jipu hili la pikipiki pale mjini hulitumbui? Kwa sababu hali hii ikiendelea ni sawa na ubaguzi.”

Pamoja na agizo hilo Mrema amesema “sina nia ya kumfitinisha Makonda bali inachotaka kuona ni utendaji wa kazi unaozingatia haki kwa madereva hao.

error: Content is protected !!