January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mrema ageukwa TLP

Mwenyekiti wa TLP Augustine Mrema akifungua mkutano mkuu.

Spread the love

LICHA ya tambo za Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Taifa, Augustine Mrema kuwa ameombwa na Kamati Kuu kutetea nafasi yake katika uchaguzi unaofanyika leo, baadhi ya wanachama wanapinga mkutano mkuu wakidai wajumbe wake sio halali.Anaandika Pendo Omary… (endelea)

Mkutano huo, unafanyika katika Hoteli ya Kings Palace iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam ambapo kwa mujibu wa Mrema, wajumbe 120 kutoka mikoa yote nchini walitarajiwa kuhudhuria.

Hata hivyo, kauli ya Mrema inakinzana na baadhi ya wanachama wa TLP ambao wamekuwa wakipingana naye kwa muda mrefu hadi kufikia hatua ya kuwasilisha malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Akizungumza na MwanaHALISIOnline kwa niaba ya wenzake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya TLP, James Haule amesema “kinachofanyika leo sio mkutano mkuu labda kama ni genge la watu wako kwenye harusi.”

Haule anafafanua kuwa “hatukushirikia mkutano huo kwa sababu hauna wajumbe halali. Ili uweze kuwa mjumbe wa mkutano mkuu kwa mujibu wa katiba ya TLP lazima uwe umechaguliwa na mkutano mkuu wa mkoa. Hili halikufanyika, sasa wanachagua nini?”

Anasema kuwa hayo ndiyo malalamiko waliyofikisha kwa msajili wa vyama kuhusu mgogoro ndani ya TLP na hivyo Mrema akaagizwa kuhakikisha uchaguzi mkuu wa viongozi wa chama unafanyika kabla ya Aprili 24 mwaka huu.

Alipoulizwa kama wamelalamika tena kwa msajili kuhusu uhalali wa wajumbe wa mkutano unaoendelea. Haule amesema “Msajili anatuhadaa kwamba kama hatukubaliani na uchaguzi tufungue kesi mahakamani, huku akijua kabisa kwa mujibu wa katiba ya TLP, mwanachama akienda mahakamani anajifuta uanachama.”

“Sisi tunamtaka msajili wa vyama awajibike kwa hili, ajiuzulu kwa sababu ndiye anambeba Mrema kukiuka katiba. Mimi naishi hapa Dar es Salaam, hao wanaoitwa wajumbe wa mkutano mkuu ni ‘wahuni’ wa kuokoteza mitaani wamelipwa posho na kupewa kofia na fulana,” amesema Haule.

Akijibu tuhuma hizo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa TLP, Mrema amesema “kumezuka kikundi kinachojiita Kamati ya Maridhiano ndani ya TLP, ambacho kinapinga uhalali wa marekebisho ya katiba ya chama hicho ya mwaka 2009, uhalali wa uongozi uliopo madarakani na madai ya kukiukwa kwa katiba.”
Mrema ambaye alitumia takribani asilimia 90 ya hotuba yake kulalamika kwa wajumbe kwa masuala yake binafsi ya ubunge wa Vunjo, amedai kwamba TLP ina migogoro ya aina mbili- moja ni ile inayohusu chama kwa ujumla wake na ule unaomhusu yeye pekee.

Amesema mgogoro unaomhusu yeye pekee ni dhidi ya Abdulrahman Kinana – Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na James Mbatia – Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi.
Mrema amesema 25 Machi 2015, Kinana alimkashfu na kumchafua na kumsingizia tuhuma za uongo kwamba anajilimbikizia madaraka yote, hakuna wa kumhoji na ni Mwenyekiti wa fedha za mfuko wa jimbo.

Ameongweza kuwa, kumekuwepo na kampeni chafu ya kukifuta TLP kwenye jimbo la Vunjo na nchi nzima. Kampeni alizodai kufanywa na NCCR – Mageuzi chini ya Mbatia; zilizopewa jina la “Delete TLP/Mrema”.
“Aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi, Makao makuu ya TLP, Getrudi Pwillah, aliasi na kujiunga na

NCCR – Mageuzi na yeye ndiye kuanzia wakati huo amekuwa kinara wa kampeni ya Delete TLP,”amedai.
Kwa mujibu wa Mrema, mgogoro mwingine ni kuhusu Jeremiah Shelukindo – aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho na kuasi kisha kuzira kuingia ofsini na kukataa kufanya kazi za chama.

Amesema “kuna baadhi ya viongozi wa mikoa wakiwemo madiwani hawafanyi kazi za chama na wamejiunga kwa siri/wazi na njama za “Delete TLP”.Ushahidi uliopo, madiwani Yolanda Lyimo wa kata ya Kilema Kati na Jesse Makundi wa Mwika Kaskazini, walinukuliwa na gazeti la Tanzania Daima la Oktoba 2014 wakimpigia debe waziwazi jukwaani Mbatia.”

Mrema pia amezungumzia hali ya ulinzi na usalama nchini kwa kusema kwamba hali ya siasa nchini sio nzuri, kutokana na kuwepo matukio ya ugaidi, udini, mauaji ya albino, uvamizi wa vituo vya polisi na migomo isiyokwisha.

error: Content is protected !!