July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mramba, Yona jela miaka mitatu, Mgonja huru

Waziri wa Fedha Basil Mramba (kushoto) na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam imewahukumu aliyekuwa   Waziri wa Fedha Basil Mramba na  aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona  kwenda jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia  ya matumizi mabaya ya madaraka kesi  iliyokuwa inawakabili. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Aidha, Mahakama hiyo imemuachia huru  aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Aggrey Mgonja kwa kutopatikana na hatia hukumu ambayo imesomwa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi  Sam Rumanyika.

Aidha, Mramba amehukumiwa kwa makosa yote 11, ambapo, kosa la 1-10 adhabu yake ni kifungo cha miaka mitatu, na kosa la 11 adhabu yake ni kifungo cha miaka mitatu au faini ya pesa shilingi milioni tano.

Nae Yona, amekutwa na hatia ya kosa la 1-5 ambapo yanadaiwa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha hivyo kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu na kosa la 11 ni adhabu ya miaka mitatu au faini ya pesa shilingi milioni 5.

Vigogo hao  walishitakiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya, kuibeba kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation ya Washington DC, Marekani ambayo ilikuwa ikifanya kazi ya uhakiki wa mapato ya madini ya dhahabu nchini.

Pamoja na kutoa upendeleo wa kuongeza mkataba wa kampuni hiyo ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation, Mramba na Yona wakiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Nishati na Madini, waliisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 11 kutokana na kusamehe kodi kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Makosa hayo ambayo yalielezwa mahakamani hapo kutendwa katika kipindi cha mwaka 2002 na mwaka 2007, ambako Mramba aliandaa na kutoa matoleo ya Gazeti la Serikali (GN) yenye namba 423/2003, 424/2003, 497/2004, 498/2004, 377/2005 na 378/2005 ambayo yalilenga kutoa msamaha wa kodi kwa Alex Stewart (Assayers) Government BC uliofikia kiwango cha Sh 11, 752, 350, 148/- bila kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa mamlaka yao na nafasi zao, Mramba na Yona wamedaiwa mahakamani hapo kwamba bila kuzingatia wajibu wao waliokabidhiwa na serikali waliingia mkataba ulioisababishia serikali hasara ya  Sh 11, 752, 350, 148/- kutokana na kampuni hiyo ya uhakiki wa dhahabu.

Imedaiwa kwamba Mramba kupitia matoleo mbalimbali ya Gazeti la Serikali amewezesha kutolewa kwa msamaha wa kodi ya mapato iliyopaswa kulipwa na kampuni hiyo ya Alex Stewart kinyume cha sheria ya Kodi ya Mapato.

Kwa mujibu wa maelezo ya waendesha mashitaka hao, Mramba anadaiwa alitumia vibaya madaraka yake kwa kudharau ushauri wa TRA waliomtaka kutokubali kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa kampuni hiyo ya kigeni ambayo ililalamikiwa sana kwa kumega mapato ya dhahabu nchini.

Mawaziri hao wa zamani wanatuhumiwa pia kudharau maelekezo ya kamati ya ushauri ya serikali ambayo ilipendekeza kupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkataba wa Alex Stewarts na badala yake waliongeza muda wa mkataba wa kampuni hiyo bila kuzingatia suala la kupitia upya ada iliyokuwa ikilipwa kwa kampuni hiyo na hivyo kuiingizia serikali hasara.

Katika kuongeza mkataba huo, Mramba na Yona wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kumshirikisha Dk. Enrique Segura wa Alex Stewarts katika kuingia naye mkataba wa nyongeza ya miaka miwili kuanzia Juni 14, 2005 hadi Juni 23, 2007 bila kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2002 na Sheria ya Madini ya mwaka 2002.

Mashitaka dhidi ya watuhumiwa hao yamefuatia kibali kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Elieza Feleshi kutoa kibali,  Jumatatu akisema kwamba viongozi hao waandamizi wametumia vibaya madaraka yao na wamesababisha hasara kwa mamlaka husika.

Hatimaye leo  hukumu hiyo  ulioyokuwa ikisubiriwa kwa hamu baada ya kupigwa danadana mara mbili  umetimia na kutolewa kwa hukumu hiyo.

Leo, watuhumiwa hao wote wawili, hakuweza kupata fursa ya kuongea tena na ndugu wala jamaa, badala yake walikuwa chini ya ulinzi mkali hadi walipoanza msafara wa kuelekea  gerezani wakiwa kwenye difenda ya polisi.

Hali ilivyokuwa mahakamani

Mahakamani hapo kulikuwa kumefurika na wakazi wengi wakiwemo ndugu na jamaa zao huku wakishindwa na mke wake Mramba alishindwa kujizuia na kumfuata kizimbani huku akibubujikwa na machozi. 

Mgonja baada ya kuachiwa huru familia yake  wakiwemo ndugu na jamaa zake walipanda kwenye gari  lao na kuondoka eneo la mahakamani hapo.

error: Content is protected !!