October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mradi wa kuzalisha majani bora ya kulishia mifugo wazinduliwa

Spread the love

TAASISI ya tafiti za mbegu bora za mazao (TARI) katika kituo cha Hombolo kwa kushirikiana na Shirika la Advanta Seed International kinatekeleza mradi maalumu wa kutafiti na kuzalisha mbegu bora za malisho ya wanyama (Mifugo). Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mradi huo wa mwaka mmoja ambao kwa sasa umefikia hatua nzuri unajihusisha na tafiti za mbegu bora za malisho za mazao ya mtama na uwele.

Mzalishaji Mbegu Mkuu wa kituo hicho, Dk. Lameck Nyaligwa amesema mradi huo unatarajia kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya mifugo hapa Tanzania.

Aidha, amezitaja baadhi ya aina za mbegu za mtama ambazo zipo katika mashamba hayo ya majaribio kuwa ni pamoja na Sugar –Grace, Mega-Sweet, BMR Rocket na Jumbo-Gold.

“Mbegu hizi zinazalisha majani na miti yenye virutubisho muhimu sana kwa ajili ya malisho ya wanyama, hususan katika kuongeza uzito wa mnyama pamoja na uzalishaji wa maziwa,” alieleza Dk. Nyaligwa.

Pamoja na hayo, amesema mradi huo utakapopitishwa na wataalamu unaongeza fursa za kiunchumi miongoni wa wakulima, wafanyabiashara na wafugaji. 

“Mradi huu utakapopitishwa utatoa fursa kwa wakulima kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania kuja kununua mbegu husika na kwenda kuzalisha malisho haya ya kisasa na kuyauza kwa wafugaji, hali ambayo itawaongezea kipato,” alisema Mtafiti huyo.

Akieleza fursa nyingine inayotarajiwa kuzalishwa na mradi huo muhimu, Dk. Nyaligwa alisema kituo kitafungua milango kwa makampuni makubwa hapa nchini kwenda kununua mbegu hizo kwa ajili ya kuzilima katika mashamba makubwa na baadae kuyasindika majani hajo ili waweze kuyauza katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Naye Diwani wa kata ya Hombolo Bwawani,  Ased Ndajilo alisema mradi huo unatarajia kuleta mapinduzi makubwa kwa wafugaji na wakulima Tanzania.

Naye Monica Malundo ambaye ni mkazi wa kata ya Hombolo Bwawani alisema mfumo wa mazao ya malisho yatapunguza kasi ya ufugaji wa kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho mbali.

Kwa upande wake, Joseph Mwaja ambaye ni mfugaji katika kata ya Hombolo Bwawani, alisema mazao ya malisho yatakuwa mkombozi kwa wafugaji kwani wataongeza wingi wa mazao ya mifugo ikiwa ni oamoja nakupata maziwa mengi.

error: Content is protected !!