October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mpina aibu mapya ucheleweshwaji Bwawa la Nyerere, amgomea waziri

Spread the love

 

MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) amefichua kuwa moja ya sababu iliyochelewesha Bwawa la Nyerere kutojazwa maji kwa muda uliopangwa ni mkandarasi wa ujenzi wa bwawa hilo kukaidi kuzingatia usanifu wa mradi huo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mpina ametoa kauli hiyo leo tarehe 2 Februari, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akiuliza swali la nyongeza kuhusu kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere.

Kwa kuwa mkandarasi huyo alitakiwa kujaza maji kwenye bwawa hilo hadi kufikia tarehe 15 Novemba mwaka jana, Serikali imesema janga la Corona ndiyo sababu iliyomfanya mkandarasi huyo kuchelewa kujaza maji hayo.

Aidha, Mpina alikataa majibu hayo ya Serikali na kusisitiza kuwa Waziri wa nishati alifika mbele ya Kamati ya Bunge ya Bajeti Novemba mwaka jana na kusema sababu ya mradi kuchelewa ni mkandarasi kukaidi design iliyowekwa na watalaam.

“Design iliyowekwa ilikuwa ya kujenga mahandaki matatu kwa ajili ya kuchepusha maji badala yake mkandarasi alijenga handaki moja jambo ambalo lilimfanya achelewe sana kukamilisha kazi hiyo, kwa hiyo ndio sababu kubwa ya msingi.

“Sababu kuwa ya UVIKO zilikataliwa, leo wamekuja na majibu mengine, wanasema ni kuchelewa kwa mitambo ya kubebea vyuma, sasa majibu yanajikanganya. Walisema watampiga penalty kwa ucheleweshaji huu… nini majibu ya serikali ya kuchelewesha mradi huu? Alihoji Mpina.

Katika swali la msingi Mpina ameuliza Je, ni sababu gani zilizopelekea kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere, kwanini Mkandarasi ameshindwa kujaza maji kwenye Bwawa kufikia tarehe 15 Novemba, 2021 kama ilivyokuwa imekubalika.

Pia aliuliza, Je, ni hatua gani zimechukuliwa kutokana na ucheleweshwaji huo.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema muda wa kukamilika kwa mradi kimkataba ni tarehe 14 Juni, 2022 hivyo tarehe hiyo bado haijafikiwa.

Amefafanua ili bwawa la Julius Nyerere lianze kujazwa maji, ni sharti liwe limejengwa kufikia kimo cha mita 95 juu ya usawa wa bahari ambapo kazi hiyo imekwishakamilika.

Amesema ilitakiwa handaki lililojengwa kuchepusha maji ya mto Rufiji kuzibwa.

“Kazi ya kuziba/kufunika handaki kwa kutumia vyuma maalumu vizito ilihitaji mfumo maalumu wa kudumu wa mitambo ya kubebea milango hiyo (Hoist Crane system) kuwepo katika eneo la mradi.

“Mfumo huo unatengenezwa mahsusi kwa ajili ya kazi hii na kazi inapoisha crane hizo huondolewa na hautumiki kwa kazi nyingine,” amesema.

Ameongeza mitambo hiyo ilichelewa kufika kwa wakati kutokana na viwanda kufungwa na safari za meli kuathiriwa kutokana na UVIKO 19 lakini sasa milango na mtambo wa kubebea tayari imefika na kazi za kuifunga zinatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2022.

“Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO inaendelea kumsimamia mkandarasi aongeze kasi ya utekelezaji wa ujenzi ili kufidia muda uliopotea kwa kuongeza wafanyakazi na muda wa kazi,” amesema.

Baada ya kutoa majibu hayo, Mpina alipata nafasi ya kuuliza swali hilo la nyongeza na kusema kwa majibu hayo mradi huo wa kufua umeme hauwezi kukamilika kama mkataba ulivyosema.

Hata hivyo, Byabato alirejea na kusisitiza kuwa kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika tarehe 14 Juni 2022.

“Wazungu wanasema ‘do not cross the river before you reach there’… kwa hiyo muda utakapofika kama mradi haujakamilika hatua za kimkataba zitachukuliwa kwa aliyesababisha ucheleweshaji,” amesema Naibu Waziri huyo.

error: Content is protected !!